Nchimbi azikataa Simba,Yanga

Muktasari:

Staa huyo wa zamani wa Njombe Mji alijipatia sifa baada ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kupiga ‘hat- trick’ katika pambano dhidi ya Yanga. Alikiri kwamba kuna viongozi wa timu kubwa wanamfukuzia.

MSHAMBULIAJI anayekuja juu kwenye kikosi cha Taifa Stars, Ditram Nchimbi amedai anataka kwenda nje ya nchi pindi mkataba wake na Azam FC ukifika tamati mwisho wa msimu huu.

Nchimbi ambaye bao lake la ushindi kwa Stars dhidi ya Sudan liliipeleka Stars kwenye fainali za CHAN baada ya miaka tisa, ameanza kutajwa kutakiwa na klabu kubwa za Simba na Yanga.

Kwa sasa staa huyo anakipiga kwa mkopo Polisi Tanzania lakini amekuwa katika kiwango kizuri kiasi cha kuitwa kikosi cha Stars chini ya kocha Etienne Ndayiragije.

“Mkataba wangu na Azam unamalizika Juni. Wamenipigia niongeze mkataba lakini sifikirii kufanya hivyo kwa sasa. Natamani sana kucheza nje,” alisema Nchimbi.

“Unajua nimecheza klabu tano za Ligi Kuu na sasa nataka kucheza nje. Kwa hapa nchini mimi naona imetosha aisee,” aliongeza Nchimbi.

Staa huyo wa zamani wa Njombe Mji alijipatia sifa baada ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kupiga ‘hat- trick’ katika pambano dhidi ya Yanga. Alikiri kwamba kuna viongozi wa timu kubwa wanamfukuzia.

“Ni kweli lakini kama nilivyosema, naweza kuacha mkataba wangu ufike mwisho nikacheze zangu nje,” alisema.