Nchimbi ataja kinachomkwamisha Yanga

Muktasari:

Awali, Nchimbi alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji wa kati, lakini Eymael alimsogeza kucheza pembeni

WAKATI mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi akikiri kushindwa kufikia malengo aliyojipangia kwa msimu huu, ameeleza sababu kubwa kuwa ni kocha wake Luc Eymael kumbadilisha namba yake kucheza.

Awali, Nchimbi alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji wa kati, lakini Eymael alimsogeza pembeni kitendo kilichomfanya kushindwa kufikia malengo yake.

“Nikicheza katikati uwezo wa kufunga unakuwa mkubwa tofauti na nikicheza pembeni, natakiwa kutoa pasi kwa wenzangu kufunga, muda mwingine unaweza kutoka uwanjani ukaangalia mechi marudio ukajiuliza hivi pale nilishindwa kufunga kweli, lakini ndio hivyo mpira na maelekezo ya mwalimu lazima yafuatwe.

“Sasa sina uwezo wa kumkatalia kocha kwa kuwa ndiye kaamua kunipanga pembeni, lakini kusema ukweli ni sehemu ambayo inakuwa ngumu kwangu kuonyesha vitu vyangu jamani,” alisema mchezaji huyo aliyewika na Polisi Tanzania

Mwanaspoti ilimtafuta Eymael akasema; “Mimi kama kocha nimeona akicheza pembeni anakuwa bora tofauti na akicheza katikati, ndiyo sababu ya kumtumia katika nafasi hiyo kwa msaada wa timu pia.”