Natasha amemsahau Khadija Nito

Muktasari:

Msanii huyo awali alikuwa akitumia jina la Khadija Nito lililomtambulisha katika tasnia ya muziki nchini sasa ameamua kubadili staili ya maisha yake kwa kuokoka na kubadilisha jina lake hadi kazi.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Khadija Nito aliyetamba na wimbo wa 'Maumivu' ameamua kubadili kilakitu katika maisha yake mara baada ya kuamua kuokoka na sasa anaitwa Natasha Lusimo.
Natasha alisema hajutii kuhamishia majeshi yake katika muziki wa Injili na anaamini kuwa tangu ameingia katika tasnia hiyo anaamani ya moyo kwa sababu anaimba kwa kumaanisha.
Natasha alisema japo alipata shida kujitambulisha upya kwa jina jipya, anajivunia kuhamia kwenye muziki wa sasa kwa sababu, anaamani na kile anachokiimba.
"Unajua kule unaimba lakini kile unachokiimba unaweza usikifanye kwa vitendo lakini huku ninachokiimba namaanisha," alisema mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na nyimbo za 'Si ulisema' 'Maumivu' lakini sasa amejizolea umaarufu kwenye muziki wake mpya baada ya kufanya Cover la Goodluck Gozebert la 'Shukrani'.
"Kwa mara ya kwanza nimeamua kuimba muziki wa injiri nilianza kufanya Cover ya Gozebert namshukuru Mungu nimefanya vizuri na nilipokelewa vizuri na wadau wa muziki huo, lakini kikubwa zaidi ni kupewa nafasi ya kufanya wimbo huo na muhusika."
Natasha alisema baada ya kupokelewa vizuri katika tasnia ya muziki huo aliamua kuachia kazi mpya inayokwenda kwa jina la Mfariji anamshukuru Mungu unafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya radio.