Natamani kuyaona haya kwa Kaze

Wednesday October 21 2020
kocha kaze pic

KAULI kutoka kwa uongozi wa hususan wadhamini wetu, GSM, ni kwamba wametuletea kocha Cedric Kaze ambaye ni raia wa Burundi kuifundisha klabu yetu ya Yanga huku wakituhakikishia kwamba huyu kocha ni fundi wa mpira na ndani ya muda mfupi tutafurahi.

Ni lazima tukiri kama mashabiki na wanachama tuna kiu kubwa kuona timu inapata kocha mzuri anayejua kufundisha soka la kisasa na tukaendelea kufurahia timu iliyosajiliwa msimu huu. Kwanza kabisa niwapongeze uongozi na zaidi GSM kama wadhamini na wote walioshiriki kututengenezea timu bora ambayo mpaka sasa imethibitisha ubora wake uwanjani kwa kushinda mechi nne na kutoka sare moja.

Tunafahamu kwamba hatua hii sio rahisi ni ngumu na yenye kuhitaji gharama kubwa ndani yake, na sasa hitaji kubwa ni kuwa na kocha mzuri.

Hatukatai ni kweli kwamba kocha aliyepita Zlatko Krmpotic alifanya kazi yake kwa kiwango chake, na ni lazima tumshukuru kwa kutupa matokeo mazuri, lakini ukweli bado hatukuwa tunacheza mpira mzuri sana, ila tunashinda lakini presha ilikuwa kubwa.

Sasa uongozi umetuletea Kaze. Binafsi simjui kabisa lakini kwa sifa zake nikilisoma gazeti pendwa la Mwanaspoti naona ni kocha mzuri - basi natamani kuyaona kwake yafuatayo:

MPIRA WA UFUNDI MKUBWA

Advertisement

Nimefuatilia kwenye mitandao nimegundua kwamba ni fundi sana wa kusoma mpira. Hili ni jambo la kwanza ambalo natamani kuliona mara tu Kaze atakapojitokeza mbele yetu akiwa na Yanga yake pale uwanjani. Tunaambiwa amekuwa akifanya kazi na akademi za Barcelona na mpaka anapata kazi hapo ina maana wanajua ana kitu kulingana na falsafa ya soka ya klabu hiyo kubwa duniani.

KUIUNGANISHA HARAKA TIMU

Makocha waliopita walikuwa wanasema muunganiko wa timu bado na hili limekuwa likitumiwa hata na watani wetu kutucheka pale wanaposhinda wakituambia sisi bado tunatafuta muunganiko. Huu ni mtihani mwingine kwa Kaze nasubiri kuona analitatua hili haraka.

Kwa mechi za kwanza tutamvumilia kwanza kwa vile tayari mwanzoni tulishafanya kosa tukamuweka Mserbia ambaye alitupotezea muda na akatuingiza pia kwenye hasara.

SOKA LA KUVUTIA

Kaze lazima akumbuke kwamba kocha aliyepita sio kwamba alikuwa hashindi, alikuwa anapata matokeo, lakini ushindi wake hauvutii kabisa tulikuwa tunashinda goli moja.

Labda katika mechi yake ya mwisho alishinda zaidi, lakini sasa tunataka kuona tunatamba mbele ya watani zetu kwa kushinda sio tu mabao mengi, lakini pia mpira wa kuvutia ndani yake kwa kuwa wachezaji bora tunao.

Pia, bado safu ya ushambuliaji sio kali. Kuna washambuliaji wawili tu wamefanikiwa kufunga tena bao mojamoja ambao ni Yacouba Sogne na Michael Sarpong.

Hii sio kasi nzuri sana, kwani kunaonekana bado kuna kitu cha ufundi kinatakiwa kufanyika na hii ni changamoto nyingine ya Kaze ili tujue tuna washambuliaji wazuri au bado tunatakiwa kutafuta watu bora zaidi. Ana mtihani mkubwa wa kutupa ule mzuka uliotufanya tujazane pale kwenye Uwanja wa Ndege kuwapokea hao wachezaji. Tunawapenda lakini hawajatupa utamu, Kaze tumia ujanja wako tufurahi.

YANGA INATAKA MATAJI

Juu ya yote msimu huu Yanga inataka mataji. Ni muda wa misimu minne sasa klabu kubwa kama haina mataji.Hili linaweza kuwa kubwa zaidi Kaze atatukosha mioyo yetu kama ataweza kutuondoa kwenye kiu hii tukipata makombe yote ya ndani. Haya yatakuwa mafanikio makubwa, ila akikosa angalau tupate moja. Tupate angalau kitu cha kubishana, kwani huku mtaani Simba wanaongea sana. Hatupumui. Wakibeba tena safari hii watatuhamisha nchi hawa ndugu.

TUFUNGIE SIMBA

Kibarua kingine kwa Kaze ni kuifunga Simba. Msimu uliopita walitufunga vibaya, hakuna shabiki, mwanachama wala kiongozi atakayesahau kirahisi matokeo yale. Inawezekana ndio kikubwa kilichochea wadhamini wetu GSM wakafanya usajili huu mkubwa na pia akatafutwa Kaze. Ni matarajio yetu kwamba ujio wake utakuja kumaliza ufalme wa Simba ambao wanajiona wako juu.

KUIRUDISHA YANGA KIMATAIFA

Msimu huu hatutakuwa katika mashindano ya kimataifa kutokana na msimu uliopita haukuwa na matokeo mazuri kwetu. Tunatamani kuona Kaze aturudishe kwenye anga za kimataifa msimu unaokuja na msingi wa hilo ni kuchukua mataji au taji moja msimu huu, kwani Yanga sio timu inayotakiwa kuwa na ushindani wa ligi ya ndani pekee hasa kwa msimu wa pili mfululizo.

TURUDISHE UWANJANI

Katika miezi ya karibuni idadi ya mashabiki wa Yanga viwanjani ilikuwa imeanza kupungua. Bila hata ya kutafuna maneno sababu kubwa ilikuwa ni udhaifu wa timu na kutokuwa na uhakika na ushindi hata kama tunacheza na timu ya kawaida. Lakini hata baada ya kufanya usajili mpya bado hatujajiamini. Huo ndio ukweli, tunaenda tu kwa kupeana mizuka na wengine wanapiga hata kilevi ili kupunguza aibu kama chochote kikitokea mbele yao.

Kaze leta soka la maana na matokeo tupate mzuka ili turudi uwanjani kama wenzetu wa upande wa pili. Wanaongea sana huku mtaani. Nimalizie tu kwa kumkaribisha Kaze, lakini pia tunamtakia kila la heri katika kazi yake hapa nchini.

Karibu kwenye timu ya Wananchi kocha Kaze. Mimi ni shabiki wa Yanga

Advertisement