Nataka kuwa mwisho kuishangilia Stars

Muktasari:

Kawaida yetu tunapenda kufaidika na ushindi wa Stars utasikia mengi mazuri pamoja na kuwaja presha wachezaji wetu wasizoweza kuzimudu na matokeo yake tutayaona mwisho.

Dar es Salaam. Nataka kuwa mwisho kushangilia, ndiyo nataka kuwa wa mwisho kabisa kushangilia ushindi wa Taifa Stars uliotoa matumani ya Tanzania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2019, Cameroon.

Taifa Stars ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde kwenye Uwanja wa Taifa, na kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 3-0 ugenini Praia.

Ushindi huo wa Stars umeifanya kufikisha pointi 5, ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara Uganda wenye pointi 10, huku Cape Verde ya tatu na pointi nne na Lesotho inashikiria mkia ikiwa na pointi mbili.

Hali hiyo tayari imeanza kuwaaminisha baadhi ya wadau wa soka kuwa Tanzania inaweza kufuzu na kucheza AFCON2019 kwa sababu wanamechi moja dhidi ya Lesotho ugenini moja ya timu dhaifu katika kundi kabla ya kurudiana na Uganda kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni mechi ya mwisho.

Ukiangalia kihesabu ni kama Stars imefuzu kwa sababu tunaamini Uganda ataifanya kazi yetu kwa kumfunga Cape Verde hivyo atakuja Dar es Salaam kutembea katika mechi ya kukamilisha ratiba.

Baada ya kuifunga Cape Verde na Lesotho kufunga 3-0 na Uganda nyumbani kwake kuna watu wameanza kuamini Stars inakwenda kuchukua pointi tatu kirahisi pale Novemba 16 nchini Lesotho, huku tukiamini kwa kuwa Uganda amefuzu atacheza kwa lengo la kutubeba.

Pamoja na mazingira hayo bado nataka kuwa wa mwisho kuishangilia Taifa Stars ikifuzu kwa Afcon 2019 kwa sababu ya rekodi na historia ya timu yetu.

Tangu 2008 hadi sasa Tanzania imeshindwa kufuzu kwa Afcon kwa sababu ya makossa madogo ya kiongozi hasa suala la kushindwa kuwaanda kisaikolojia wachezaji wetu wanapokuwa wamepewa matumaini makubwa ya kufanikiwa.

Mfano wa karibuni kabisa ni kipigo cha mabao matatu Stars ilichopata Cape Verde wiki iliyopita kilitokana na wachezaji wa uongozi kwenda kule wakiwa wanajiamini wanakwenda kushinda kilichotokea ni aibu.

Kufuzu 2008, Ghana

Juni 16, 2007, Tanzania ilifanya maajabu baada ya Stars kuichapa Burkina Faso kwa bao 0–1, shukrani kwa bao pekee la beki Erasto Nyoni dakika ya 77, kwenye Uwanja wa 4-Aout, Ouagadougou.

Baada ya ushindi huo Stars ilifikisha pointi 8, hivyo kuhitaji sare ya aina yote au ushindi dhidi ya Msumbiji katika mchezo wa nyumbani ili kufuzu kwa Afcon 2008.

Zikatungwa nyimbo zikapigwa, ngonjera na shangwe za kila namna tukiamini Msumbiji hapa hatoki ukizingatia tulipata suluhu kwake.  

Nakumbuka Septemba 8, 2007, kila Mtanzania alikuwa anaamini Stars inashinda mchezo wake dhidi ya Msumbiji na kufuzu kwa Afcon2008, Ghana.

Kabla ya mchezo huo Stars ilikuwa nafasi ya pili katika Kundi L ikiwa na pointi 8, na Msumbiji ikiwa ya tatu na pointi 7. lakini bao la dakika ya nane la Tico-Tico lilileta majonzi kwa taifa zima.

Kundi 7

                     Pld  W     D       L        GF    GA    GD    Pts

 Senegal          6          3       2       1       12     3       +9     11

 Msumbiji         6       2       3       1       5       4       +1     9

 Tanzania        6          2       2       2       4       7       −3     8

 Burkina Faso   6       1       1       4       5       12     −7     4

 

Tanzania 2–1  Burkina Faso

Msumbiji 0–0  Tanzania

Senegal    4–0  Tanzania

Tanzania 1–1  Senegal

Burkina Faso    0–1  Tanzania

Tanzania 0–1  Msumbiji

Kufuzu Afcon2010, Angola

Tanzania ikiwa Kundi 1, pamoja Cameroon, Cape Verde na Mauritius kila mtu aliamini kwa kundi hilo yale makosa ya 2008 hayatajirudia kutokana na udhaifu wa timu hizo ukitoa Cameroon.

Stars ilifanya kosa la kiufundi ilikubali kulazimishwa sare 1-1 na Mauritius kwenye Uwanja wa Taifa, huku Emmanual Gabriel akikosa penalti iliyokuwa kama pigo kwa Tanzania.

Katika kundi hilo Stars ilifungwa mechi mbili zote ugenini dhidi ya Cameroon na Cape Verde, ikitoka sare mbili na kushinda mbili ikakusanya pointi nane

Kundi 1

                         Pld       W     D       L        GF    GA    GD    Pts

 Cameroon       6       5       1       0       14     2       +12  16

 Cape Verde     6       3       0       3       7       8       −1     9

 Tanzania        6          2       2       2       9       6       +3     8

 Mauritius         6       0       1       5       3       17     −14  1

Matokeo

Tanzania 1-1 Mauritius

Cape Verde 1-0 Tanzania

Tanzania 0-0 Cameroon

Cameroon 2-1 Tanzania

Mauritius 1-4 Tanzania

Tanzania 3-1 Cape Verde

Kufuzu Afcon 2012, Gabon, Equatorial Guinea

Taifa Stars ikiwa Kundi D chini ya kocha Jan Poulsen ‘babu’ iliushangaza ulimwengu baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Algeria ugenini ikaichapa Jamhuri ya Afrika Kati mabao 2-1 Dar es Salaam.

Kama kawaida yetu baada ya ushindi huo wachezaji na Watanzania tukaanza kujiaminisha kwamba Afrika Kati ni vibonde wetu tukaenda kwao tukiwa na imani kubwa ya kushinda, lakini tulipoenda huko tukachapwa 2-1, mwisho Stars ikamaliza ya mwisho ikiwa na pointi tano.

Kundi D

         Pld   W     D       L        GF    GA    GD    Pts

 Morocco 6       3       2       1       8       2       +6     11

 C.A.R        6       2       2       2       5       5       0       8

 Algeria    6       2       2       2       5       8       −3     8

 Tanzania 6       1       2       3       6       9       −3     5

Matokeo

Algeria     1–1  Tanzania

Tanzania 0–1  Morocco

Tanzania 2–1  Central African Republic

Central African Republic 2–1  Tanzania

Tanzania 1–1  Algeria

Morocco 3–1  Tanzania

Kufuzu Afcon 2013, Afrika Kusini

Katika fainali hizi Tanzania ilianza hatua ya awali ikiwa imepangwa kucheza na Msumbiji na mshindi wa mechi hiyo anasonga mbele.

Katika mchezo wa kwanza nyumbani uliochezwa Februari 29, 2012 Tanzania ilazimishwa sare 1-1 na Msumbiji, katika mchezo wa marudiano uliofanyika Maputo ililazimisha sare 1-1 Juni 17, 2012.

Kutokana na sare hiyo ndipo penalti zikatumika kuamua mshindi na Mbwana Samatta alikosa penalti ya mwisho ya saba Stars ikitole kwa mikwaju 7-6.

Kufuzu Afcon 2015, Equatorial Guinea

Ndoto ya kufuzu kwa Afcon imeendelea kuwa ndoto pamoja na kusonga mbele kwa raundi ya awali ikifanikiwa kushinda mchezo wa nyumbani dhidi ya Zimbabwe kwa bao 1-0, na kulazimisha sare ya ugenini wa mabao 2-2.

Katika raundi ya kwanza ililazimishwa sare 2-2 nyumbani na Msumbiji kabla ya kuchapwa mabao 2-1 jijini Maputo na safari yake kuishia hapo.

Kufuzu Afcon 2017, Gabon

Fainali hizi za zilipangwa kwa kanda hivyo Tanzania kupangwa na Uganda, wakati huo Stars ikiwa chini ya kocha Martin Nooij.

Ukiwa na migogoro ya hapa na pale ndani ya TFF hasa baada ya kutimuliwa kwa kocha Kim Poulsen, Stars ilichezea kichapo cha mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Kabla ya kulazimisha sare 1-1 jijini Kampala na kuaga mashindano hayo.

Najua tumeshinda tutakuja na mipango mkakati mingi, lakini tutapofungwa utasikia kocha hafai kaishiwa atimuliwe yote kwa sababu uamuzi mwingi unafanya kwa kuangalia matakwa ya kisiasa zaidi.

Bado nataka kuwa mtu wa mwisho kushangilia Taifa Stars itakapofuzu kwa Afcon2019.