Namungo yaanza kunogewa

Muktasari:

Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thierry alisema baada ya kupanda hadi nafasi ya tatu kwa ushindi wa juzi sasa wanajipanga kuimaliza Azam iliyo katika nafasi ya pili kwa pointi 45 na kuwapumulia kwa pengo la alama mbili tu, kwani wao wakishinda watafikisha alama 43 katika msimamo.

USHINDI wa mabao 2-1 dhidi ya KMC umeifanya Namungo kunogewa na sasa imeanza kuzipigia hesabu pointi tatu kutoka kwa Azam ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Namungo iliyoiengua Yanga kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa wakilingana pointi 40, itakuwa wenyeji wa Azam wikiendi hii kwenye Uwanja wa Majaliwa, mjini Lindi. Timu hiyo inayoshiriki ligi kwa msimu wao wa kwanza, imekuwa moto wa kuotea mbali kutokana na vichapo inavyotembeza kwa wapinzani.

Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thierry alisema baada ya kupanda hadi nafasi ya tatu kwa ushindi wa juzi sasa wanajipanga kuimaliza Azam iliyo katika nafasi ya pili kwa pointi 45 na kuwapumulia kwa pengo la alama mbili tu, kwani wao wakishinda watafikisha alama 43 katika msimamo.

“Tunashukuru kwa matokeo mazuri, vijana wanapambana na wanasikiliza wanachoelekezwa, kwa sasa tunajipanga upya na mechi dhidi ya Azam Jumamosi kuhakikisha tunashinda tena,” alisema Thierry ambaye ni raia wa Rwanda aliyeongeza ishu ya ubingwa kwao ni ngumu kwa sasa.

“Simba imetuacha mbali sana, lakini lolote linawezekana kwa sababu mpira una matokeo tofauti, kama tutabahatika kuendeleza ushindi tunaweza kuwa na mabadiliko,” alisema Thierry.