Namungo waifungia safari Mbeya Kwanza

Friday February 8 2019

 

By Charles Abeil

Dar es Salaam. Homa ya pambano la Ligi Daraja la Kwanza baina ya Mbeya Kwanza na Namungo FC kesho Jumamosi imezidi kupanda baada ya kundi la mashabiki wapatao 170, kusafiri kutoka wilayani Ruangwa hadi Mbeya kwa ajili ya kuwasapoti wageni kwenye mechi hiyo.
Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu na wadau wa soka nchini kutokana na nafasi ya timu hizo mbili kwenye msimamo wa kundi A la Ligi Daraja la Kwanza.
Namungo inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi 24, wakati Mbeya Kwanza inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 23.
Ushindi wa Namungo kwenye mchezo huo utaifanya iongeze pengo kubwa la pointi baina yake na Mbeya Kwanza kufikia nne jambo litakaloiweka kwenye nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Kwa upande wa Mbeya Kwanza, ushindi dhidi ya Namungo utaifanya iwe juu ya msimamo wa kundi hilo kwa pointi mbili.
Mashabiki hao wa Namungo ambao walisafiri kwa mabasi makubwa mawili, walianza safari ya kuelekea Mbeya kuanzia jana Alhamisi saa nne usiku wakitokea Ruangwa na walifika jijini humo majira ya saa 10, jioni leo Ijumaa.

Advertisement