Namungo FC yapandisha mzuka Lindi hizi hapa sababu za kupanda TPL

Muktasari:

  • Makala hii inakuletea baadhi ya sababu ambazo pengine zimekuwa chachu kwa Namungo kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao huku ikiwa na mechi mbili mkononi.

NAMUNGO FC imepanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu ujao. Kwa watu wa mkoa wa Lindi, hii ni tukio kubwa na lenye historia ya kipekee kwa kipindi hiki na linaweza kupokelewa kama taarifa ya mtu aliyetoka kifungoni.

Hakuna namna ambayo unaweza kuzuia furaha ya wakazi wa Lindi, baada ya Namungo kupanda kwani wamesubiri kwa zaidi ya miaka 17 ya kuishi bila uwepo wa timu inayowakilisha mkoa wao tangu pale Kariakoo ya Lindi iliposhuka daraja mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mawenzi Market ya Morogoro juzi Jumatatu na kisha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kuwapatia ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kwenye mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Friends Rangers uliovunjika, timu hiyo yenye maskani yake wilayani Ruangwa, sasa imefikisha pointi 43 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye kundi A hata kama ikipoteza mechi zake mbili zilizobakia kwenye kundi hilo.

Hata hivyo, ukitazama na kufuatilia kwa ukaribu safari ya Namungo kuanzia mwanzo hadi pale ilipojihakikishia kupanda Ligi Kuu Bara, utabaini mafanikio hayo hayakuja kwa bahati mbaya na timu hiyo ilistahili kuyapata.

Makala hii inakuletea baadhi ya sababu ambazo pengine zimekuwa chachu kwa Namungo kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao huku ikiwa na mechi mbili mkononi.

Usajili wa maana

Ubora wa uwanjani una nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya timu kwenye mashindano hata kama kuna maandalizi na mipango mingi ya nje ya uwanja kama ya kiutawala na hamasa. Namungo waligundua hilo mapema kwa kufanya usajili makini wa wachezaji ambao, wana kiwango bora na wanaojitolea ndani ya uwanja na hapana shaka wametoa mchango mkubwa kama ilivyotarajiwa.

Usajili wao ulizingatia mahitaji ya kitimu, ulikuwa na mchanganyiko ukiwahusisha wale wenye uzoefu na wengine ambao wana kiwango kizuri wengi wao wakiwa ni vijana wenye kiu ya mafanikio tofauti na namna vikosi vya baadhi ya timu vilivyoundwa na haikushangaza kuona wakiwa wamepoteza mchezo mmoja tu hadi sasa.

Benchi imara la ufundi

Namungo ilikuwa na mapungufu kadhaa ya kiufundi katika mechi za mwanzoni za Ligi Daraja la Kwanza hasa kwenye safu yake ya ushambuliaji ambayo yaliifanya iwe inapata wakati mgumu kwenye michezo yake.

Hali hiyo ilipelekea uongozi wake kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kumuondoa kocha Fulgence Novatus na kumuajiri raia wa Burundi, Hitimana Thierry ambaye kwa kiasi kikubwa ameibadili timu hiyo na kuifanya iwe tishio kwa timu pinzani ikicheza soka la kuvutia huku ikifunga idadi kubwa ya mabao tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.

Uongozi makini

Sifa kubwa kwanza zinapaswa kuelekezwa kwa mlezi wa Namungo, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa namna alivyoisadia timu hiyo inayotokea Jimbo la Ruangwa ambako yeye ni mbunge wake, kwa hali na mali na mfano wa hilo ni uwanja wa kisasa ambao amewajengea unaotumika kwa mechi zao za nyumbani.

Lakini, sifa za pili zinaenda kwa uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti Hassan Zidadu kwa kuhakikisha timu inapata mahitaji yote stahiki kwa wakati kama vile mishahara na posho kwa wachezaji, huduma za matibabu, malazi na usafiri.

Na hilo linajidhihirisha kwa Namungo kumiliki basi kubwa la kisasa, lakini pia imekuwa ikifikia hoteli nzuri kila inapocheza mechi za ugenini.

Maandalizi mazuri

Kabla ya Ligi Daraja la Kwanza kuanza, Namungo iliingia kambini mapema kwa ajili ya kuanza programu za maandalizi kuelekea ligi hiyo na ilicheza idadi kubwa ya mechi za kirafiki ikiwemo dhidi ya timu kubwa za Yanga na Simba, jambo ambalo liliisaidia kufahamu mapungufu yake na kuyafanyia kazi mapema.

Hamasa, umoja

Mashabiki wa Namungo hasa wale wa wilayani Ruangwa wamekuwa wakiisapoti vilivyo timu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kuishangalia pindi inapocheza nyumbani, lakini mara kwa mara wamekuwa wakisafiri kwa gharama zao kwenda kuisapoti pale inapokuwa na mechi ya ugenini.

Hili kwa kiasi fulani liliwafanya wachezaji wa Namungo kupambana ndani ya uwanja ili kulipa fadhila kwa mashabiki wao ambao wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwa ajili ya kuwashangilia.