Nahodha Nonga atangaza nidhamu kwanza Lipuli

Muktasari:

Nonga amepewa kitambaa cha unahodha baada ya Ally Mtoni Sonso kutimka katika kikosi hicho na kujiunga na Yanga kwa msimu mpya wa Ligi 2019/20.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Lipuli FC, Paul Nonga amesema anakazi kubwa kuhakikisha anaiongoza timu hiyo kuwa miongoni mwa timu bora zenye nidhamu msimu wa 2019/20.

Nonga amefunguka hayo baada ya kukabidhiwa kitambaa cha unahodha baada ya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo Ally Sonso kujiunga na klabu ya Yanga kwa msimu mpya.

Nonga alisema mbali na kuhakikisha timu yao inamaliza ikiwa ni timu yenye nidhamu bora amebainisha kuwa anakazi kubwa ya kupambana kuwasimamia wenzake waweze kuwa na lengo moja la kuifanya timu hiyo inamaliza katika nafasi tatu za juu.

"Jukumu nililopewa si langu peke yangu nahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wenzangu ili tuweze kutengeneza kitu kimoja ambacho kitakuwa bora zaidi naamini hili linawezekana kama nitapewa ushirikiano," alisema na kuongeza kuwa.

"Hakuna majukumu ambayo hayana changamoto kikubwa ni heshima na sisi ni watu wazima tunatakiwa kuheshimiana ili tuweze kufikia malengo kwa pamoja," alisema Nonga.