Nahodha Nigeria amkataa kocha

Wednesday July 10 2019

 

Cairo, Misri. Nahodha wa zamani Nigeria, Segun Odegbami amesema kocha wa timu hiyo hana sifa ya kuifundisha Super Eagles.

Nguli huyo alisema kama angekuwa rais wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFL) angemtimua kocha Gernot Rohr mapema.

Odegbami alisema angemfukuza Rohr muda mfupi baada ya mechi yao dhidi ya Madagascar waliofungwa mabao 2-0.

Nahodha huyo alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akichambua mechi za fainali hizo katika televisheni ambapo alidai kocha alipaswa kuwa mkali wakati wa mchezo. “Kocha alikuwa ametulia tu, hakuwa na presha licha ya timu kuzidiwa, kama ningekuwa kiongozi wa NFL ningemfuta kazi,” alisema Odegbami.

Alisema Rohr hakufanya uchaguzi sahihi wa kikosi chake katika mchezo dhidi ya Madagascar na hakuwa mkali kwa wachezaji wakati mchezo ukiendelea. “Nasikitika kwa matamshi haya lakini huo ndio ukweli, angalia makocha kama Jurgen Klopp, Jose Mourinho wanakuwa na wachezaji wao mkononi wa kuwabeba,”alisema Odegbami.

Advertisement