Nahimana aihofia Taifa Stars

Kipa namba moja  wa timu ya Taifa ya Burundi, Jonathan Nahimana amesema maingizo mapya ndani ya kikosi chao yanampa hofu wanapoelekea kuikablii  Taifa Stars katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Jumapili kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

 Kipa  huyo ambaye anaeidakia klabu ya Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara amesema wachezaji wengi wanaounda kikosi chao wanacheza ligi yao ya ndani nchini Burundi tofauti na Taifa Stars ambayo ina wachezaji wenye uzoefu na mechi za kimataifa.

"Kikosi chetu cha sasa kina wachezaji wengi wapya ambao wengi wao wanacheza ligi ya nyumbani Burundi hivyo hawana uzoefu wa kutosha kwenye mechi za kimataifa kwahiyo inabidi tuwe makini kutokana na wachezaji wengi wa Taifa Stars kujuana zaidi tukizubaa wanaweza kutufunga," amesema Nahimana.

Pia Nahimana amesema  anaamini siku tano za kambi jijini Dar es Salaam zitawaongezea kitu na kuufanya mchezo baina ya Taifa Stars kuwa wa kuvutia na wenye ushindani mkubwa.

"Naamini kambi yetu ya siku  tano tunaweza kutengeneza muunganiko mzuri na kupata kikosi bora ambacho kitaingia uwanjani kupambana na kuliwakilisha vyema taifa letu," amesema Nahimana.

Burundi ambayo imeweka kambi hapa nchini  kwenye hotel ya Seascape iliyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam. ina  nyota 11, wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo wakiwemo Nahimana, Nzigamasabo Steve na Bigirimana Blaise wanaoichezea Namungo FC.  

Mchezo wa mwisho uliozikutanisha timu hizo ulikuwa wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar na  uliochezwa Septemba 8 mwaka jana na kumalizika kwa sare ya bao  1-1 ndani ya dakika 90 na hivyo Taifa Stars kushinda kwa penalti   3-0.