Naftali aipigia hesabu Stars ya Misri

Monday April 8 2019

 

By Eliya Solomon

BAADA ya kutua Tusker ya Kenya nyota wa zamani wa Simba, David Naftal anaamini ana nafasi ya kuichezea Timu ya Taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’ katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), Misri.

Naftal ambaye ni kiraka mwenye uzoefu wa kutosha, aliwahi kuitwa Taifa Stars kipindi hicho akiwika na kikosi cha Simba kwenye miaka ya 2009 kabla ya baadaye kutimkia zake Bangkok Glass ya Thailand.

Kiraka huyo alisema kuna miezi michache mbele, hivyo amepanga kuitumia kama nafasi ya kuonyesha uwezo wake ili atimize ndoto yake ya kurejea Taifa Stars.

“Miaka imeenda na bado najiona nina nguvu za kuendelea kucheza, nimetoka Zambia na kurejea tena Kenya ambako nilikuwa nikicheza kwa kipindi kirefu.

“Nina ndoto ya kuichezea Taifa Stars, natambua kuna vijana wengi ambao wanafanya vizuri kwa sasa hilo halinisumbui akili, kinachonifurahisha ni kwamba siku hizi wachezaji wanaocheza soka nje ya Tanzania wameanza kuitwa,” alisema Naftal.

Akiwa na Tusker, Naftal ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo na amekuwa akitumika kama kiungo mkabaji. Nyota huyo ana uwezo wa kucheza nafasi zote za nyuma kama ilivyo kwa Erasto Nyoni.

Advertisement