Nafasi ya Ndemla, Rafael kujikomboa

Muktasari:

Kipindi hiki ambacho shughuli za michezo imesimama tangu agizo la serikali litolewa kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, klabu zimekuwa bize na ishu za usajili. Achana na sakata la kampuni ya GSM na Yanga, lililowang’oa baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. GSM ilitangaza kujiengua kwenye shughuli walizokuwa wakizifanya nje ya mkataba wao, ikiwamo ishu za usajili.

LIGI Kuu imesimama. Hata kule kwenye Daraja la Kwanza na La Pili nako hali ni hiyo hiyo. Kwa wale wanaofuatilia Ligi Kuu za Ulaya, kadhalika mambo yapo ovyo. Kama sio virusi vya korona (covid-19) kuzingua, tungekuwa tunaanza kujiandaa kushuhudia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2020. Korona imekuja kutibua mpaka kwenye mechi za makundi ya Kombe la Afcon 2021. Taifa Stars ilikuwa iwafuate Tunisia na kucheza nao Ijumaa na kuridiana nao Jumanne ijayo.

Katikati ya wiki hii, Michezo ya Olimpiki iliyokuwa ifanyike Julai mwaka huu imeahirishwa. Yaani mambo yapo vululu vululu. Inatia simanzi, kwa vile mbali na kuathari za kiafya kwa waliopatwa na ugonjwa huo ulioanzia kule Wuhan, China. Korona inatarajiwa kuleta athari kubwa kiuchumi, kwa sababu shughuli nyingi zimesimama.

Wachezaji wanaathirika. Klabu zinaathirika na hata wadhamini wa ligi mbalimbali duniani nao wanaathirika, kama ambayo serikali nazo zitakavyoathirika. Kama hakuna shughuli za kibiashara na uchumi, hakuna kodi. Huku nguvu kazi nyingi zinapukutika. Kwa hakika korona limeleta balaa! Tumuombe Mungu atulinde, sambamba na wenyewe kujilinda dhidi ya virusi hivyo kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kujikinga navyo.

Kipindi hiki ambacho shughuli za michezo imesimama tangu agizo la serikali litolewa kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, klabu zimekuwa bize na ishu za usajili. Achana na sakata la kampuni ya GSM na Yanga, lililowang’oa baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. GSM ilitangaza kujiengua kwenye shughuli walizokuwa wakizifanya nje ya mkataba wao, ikiwamo ishu za usajili.

Hilo sio ninalotaka kulizungumza. Nazungumzia usajili ulioanza kufanywa kimyakimya. Klabu zimekuwa zikichangamkia kuwapa mikataba mipya nyota wao na kuzungumza na wengine ili kuimarisha vikosi vyao. Kuna baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao ndani ya timu zao inaelekea ukingoni. Mbaya ni kwamba sio ipo ukingoni tu, lakini wamekuwa wakisugua benchi kwenye timu zao kwa muda wa mikataba yao hiyo.

Kwa namna ambavyo wachezaji hao wasivyopata nafasi kama kina Said Ndemla, Yusuf Mlipili waliopo Simba ama Andrew Vincent ‘Dante’, Ramadhani Kabwili, Rafael Daud na wengine kule Yanga na hata kule Azam na timu nyingine wapo kibao! Nani hakumbuki soka la Rafael alipokuwa Mbeya City? Nani hajui mashuti makali ya Ndemla kipindi akipewa nafasi Msimbazi? Lazima wajikomboe. Mashabiki wa soka bado wanapenda kuona vitu vyao uwanjani. Kukaa kwao benchi kunawanyima uhondo mashabiki wao. wana uwezo mzuri na kucheza kokote. Waondoke sasa!

Itashangaza sana kama hata dirisha hili la usajili lililofunguliwa mapema, litawapita wachezaji hao na kubaki katika klabu zao.

Itachekesha kama wachezaji hao watakubali kusainishwa mikataba mingine mipya ndani ya timu hizo, ili waendelee kukaa benchi. Kwa mchezaji anayejitambua na anayejali kipaji chake ni lazima, atafute timu itakayompa nafasi ya kucheza.

Ni kweli, soka la sasa ni biashara na wachezaji wanahitaji kuvuna fedha kuliko kitu kingine. Pengine hii ndio inayowafanya wengi wao kukomaa katika timu zisizowapa nafasi hasa timu kubwa, ilimradi tu wanavuna fedha hata kama wanakaa benchi. Lakini kuvuna fedha ndani ya timu bila kuitumikia ni kama mfanyakazi hewa na kunachangia kuua vipaji walivyonavyo.

Mashabiki wa soka wanafurahia mchezaji anayeitumikia timu yao na kuzipa mafanikio. Ndio maana kuna tofauti kubwa kati ya Yikpe Gnamein na Bernard Morrison mbele ya mashabiki wa Yanga. Ndio inayomfanya Luis Jose Miquissone kuwa kipenzi cha Msimbazi kuliko Shiza Kichuya ama Ibrahim Ajibu! Ni kwa vile hata kama mchezaji ana jina zuri na umbo la kuvutia kiuchezaji kama hana faida ya timu kwa maana ya kuitumikia hafagiliwi.

Inawezekana watu wa karibu wa wachezaji hao, hasa wale ambao kipindi kama hiki hujifanya ndio mameneja wao, ndio wanaotia ujinga.

Wanawataka wakatae ofa ndogo kutoka nje ya klabu zao, ili waendelee kusalia kwenye klabu za sasa kwa matarajio ya kuvuna fedha zaidi, bila kujua kama wanaviua vipaji vyao. Zindukeni la sivyo itakuwa kwenu!