Nafasi ya Mwakinyo yamtesa bondia wa Bongo Ujerumani

Muktasari:

  • Katika pambano hilo, Maono alicheza dakiza zote 30 za raundi 10 huku video zikionyesha mabondia hao wakishambuliana kwa zamu kabla ya majaji kumtangaza mwenyeji kuwa bingwa wa taji hilo la IBF kwa pointi za majaji wote watatu.

UNALIKUMBUKA lile pambano la Ujerumani ambalo, Bondia Hassan Mwakinyo ilikuwa aende kuzichapa lakini akaligomea baada ya kupanda ‘chati’ alipompiga Sam Eggington? sasa Maono Ally ndiye aliyeziba pengo la Mwakinyo kwenye pambano hilo lakini cha kusikitisha hakuweza kuitendea haki nafasi hiyo.

Awali Mwakinyo ndiye alikuwa akazichape na Mjerumani, Wanik Awdijan kuwania ubingwa wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa la Kimataifa (IBF) kwa vijana lakini jamaa akalitolea nje baada ya rekodi yake kupanda alipozichapa Uingereza kabla ya Maono kuchukua nafasi ya Mwakinyo.

Maono ambaye kabla ya kuzichapa Ujerumani alikuwa na rekodi ya kutwaa taji la dunia wa la WBC alipomchapa Luka Pupek kwa TKO raundi ya pili kule Afrika Kusini, aliambulia kipigo Ujerumani katika pambano lililofanyika juzi Jumamosi usiku.

Katika pambano hilo, Maono alicheza dakiza zote 30 za raundi 10 huku video zikionyesha mabondia hao wakishambuliana kwa zamu kabla ya majaji kumtangaza mwenyeji kuwa bingwa wa taji hilo la IBF kwa pointi za majaji wote watatu.

Wakala wa pambano hilo, Anthony Rutha alisema, Maono alicheza vizuri lakini matokeo ya pointi ni nadra kupata bondia anapokwenda kucheza ugenini.

Katika pambano hilo lililopigwa kwenye Ukumbi wa Alex Sportcentrum, mjini Bayern, Maono alionyesha kiwango kikubwa tofauti na ilivyotarajiwa kutokana na rekodi ya mpinzani wake ambaye alikuwa bondia wa 49 wa dunia yeye akiwa ni bondia wa 232 duniani.

“Amejitahidi kwa kweli ingawaje matokeo hayakuwa mazuri kwa upande wake,” alisema Rutha.