Nabeel atamba kufanya vizuri kuogelea Afrika Kusini

Muktasari:

 

  • Nabeel ambaye ni mwanafunzi wa shule ya wavulana ya  Al Muntazir ya jijini alisema kuwa amejiandaa vizuri ili kuibuka na ushindi au kuhimarisha muda wake katika mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la Ellis Park.

Dar es Salaam. Muogeleaji anayekuja juu  kwa kasi nchini, Nabeel Gahhu amepania kufanya vizuri katika mashindano ya kuogelea ya Afrika Kusini (South Africa Level 3 Regional group) yaliyopangwa kuanza Machi 28 mpaka 31 mjini Johannesburg.

Nabeel ambaye ni mwanafunzi wa shule ya wavulana ya  Al Muntazir ya jijini alisema kuwa amejiandaa vizuri ili kuibuka na ushindi au kuhimarisha muda wake katika mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la Ellis Park.

Alisema kuwa mpaka sasa amepata mafunzo mazuri kutoka kwa makocha wake wa klabu ya Dar es Salaam Swimming Club (DSC) na vile vile chini ya kocha wa Taifa wa mchezo huo, Alexander Mwaipasi.

Mbali ya Nabeel, waogeleaji wengine ambao wataunga timu ya Tanzania, Ria Save, Peter Itatiro, Natalia Ladha, Sophia Latiff, Aravind Raghavendran, Isabelle na  Niamh Powell.

“Nimejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano haya. Naishukuru shule yangu ya Al Muntazir kwa kunipa sapoti kubwa wakati nikiwa na majukumu ya kishule na mashindano pia, hii ni mara yangu ya pili kushiriki katika mashindano haya,” alisema Nabeel.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Inviolata Itatiro amesema kuwa timu hiyo itaondoka Machi 24 kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya maandalizi zaidi.

Inviolata alisema kuwa sababu ya kuondoka mapema ni kuwawezesha waogeaji wa Tanzania kuzoea hali ya hewa na vile vile kuvizoea vifaa vya kisasa vya mchezo huo.