Naamini mwarabu ameumia Diamond kumpa Tanasha prado

Monday July 15 2019

 

By Luqman Maloto

ILIKUWA bonge la burudani Mlimani City. Bahati iliyoje? Mama wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim (nasikia anapenda kuitwa Mama Dangote) na girlfriend wa supastaa huyo, Tanasha Donna (wahuni wanamwita Mama Kayaii), huadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa siku moja.

Yes, Sabasaba ya kila mwaka, Tanasha na Mama Dangote huongeza mwaka katika umri wao. Kwa matokeo hayo, hasa baada ya Diamond kufahamu kwamba Tanasha ni mjanzito wa mtoto wake ajaye wa kiume, akaamua kuangusha pati lenye viwango vya 7Star. Watu mashuhuri Bongo na nje ya mipaka walihudhuria.

Si unajua Tanasha ni wa kule anakoringia Jaguar Kigeugeu? Basi ujumbe kutoka Kenya ulihudhuria kamili kumsindikiza raia mwenzao, Tanasha. Haikuwa rahisi kumwalika Jaguar kwa sababu ya shobo zake za kutaka Wabongo wasepe Kenya, ila hakuna kilichoharibika, comedian supastaa, Eric Omondi alikula keki kwa niaba ya masupastaa wote wa Kenya. Jaguar akiwemo.

Ilikuwa bambamu mwana! Mpangilio wa sherehe ulienda shule. Kuna kamchezo kalifanywa ukumbini, Mama Dangote na Tanasha waliwekewa maboksi mengi ili wachague zawadi. Maboksi matatu tu yalikuwa zawadi. Ya kwanza nyumba, nyingine fedha Sh10 milioni, pia ilikuwepo ya safari ya kwenda Paris, Ufaransa, kwenye fungate la besidei. Sijui hiyo nitakuwa nimeiweka utamu?

Tanasha na Mama Dangote walifanikiwa kupata zawadi ya nyumba na Sh10 milioni. Safari ya Paris hawakushinda. Hata hivyo, Diamond si ndio Dangote? Naamini atawapeleka tu Paris wakale bata la besidei. Au ukipenda unaita honeymoon ya besidei. Kwani kuita hivyo ni Shi’ngapi?

Zikatolewa zawadi baabkubwa. Tanasha akapewa ndinga mpya, Toyota Prado TX toleo la mwaka 2018, vilevile Mama Dangote yeye alimilikishwa ‘brandi niuu’ Toyota Land Cruiser VX pia nakala ya mwaka 2018. Gari za kifahari sana hizi. Watu wengi wazito wanashindwa kuzimudu, lakini Chibudee amenunua mbili kwa mpigo na kuwapa zawadi mama na girlfriend wake.

Advertisement

Hapohapo kuna zawadi ya nyumba na Sh10 milioni zilibebwa ukumbini bila kusubiri. So, janki ana mkwanja usio na mawenge. Inavutia sana vijana kupata mafanikio yenye kuonekana, kwani hutoa hamasa kwa wengine kuchapa kazi ili nao wapige bao. Diamond ni kiigizo chema kwa wengine, hasa vijana kujituma kupitia vipaji vyao, vilevile kuwa na nidhamu katika utafutaji wao.

Prado TX toleo la mwaka 2018 ambalo Tanasha kapewa na Diamond kama moja ya zawadi za besidei, muongozo wa bei yake sokoni ni dola 62,000 (Sh140 milioni). Hapo hujazungumzia kodi wala usafirishaji. Hivyo, bei ya jumla mpaka kulimiki na kuanza kulipigia misele sio chini ya Sh200 milioni.

Naomba niiweke sawa; muongozo wa bei maana yake ni wastani. Kwani zipo ambazo huuzwa mpaka dola 43,000 (Sh100 milioni) na nyingine hadi dola 84,000 (Sh193 milioni). Bei hizo ni kabla ya kodi na usafirishaji. Hivyo, ndinga ya Tanasha unaweza kuiendesha Bongo kwa usawa kuanzia Sh170 milioni mpaka Sh300 milioni. Nimeweka Sh200 milioni kwa wastani.

Bei za magari ambayo Diamond aliwazawadia Tanasha na Mama Dangote hazitofautiani sana kutokana na mwongozo wa bei zake sokoni. Sasa basi, tuweke wastani kila gari Diamond lilimgharimu Sh200 milioni. Maana yake alikata Sh400 kuwapa zawadi hizo wapendwa wake, mama na girlfriend.

Mtu anayetumia pesa hivyo kwa zawadi tu maana yake ni bilionea. Tumpongeze Diamond kwa hatua kubwa aliyopiga kimaisha. Pongezi pia kwa kuwajali watu muhimu anaowapenda, mama yake na girlfriend wake.

NIKAKUMBUKA KILIO CHA MWARABU

Mwarabu Fighter ni mtu maarufu sasa. Umaarufu wake umetokana na kazi yake ya kumlinda Diamond Platnumz. Kibarua cha Mwarabu kiliota nyasi kienyejienyeji mwaka jana. Hivi sasa Mwarabu anafanya mitikasi yake binafsi na anamiliki kampuni ya ulinzi ambayo inaendelea kujitengenezea jina.

Habari ambazo zilithibitishwa na Mwarabu mwenyewe ni namna alivyotoswa na Diamond haikuwa imenyooka. Alishangaa tu haitwi kwa ajili ya kazi na muda ulipofika hakuitwa kuchukua mshahara. Mwezi ukapita, ukafuata wa pili. Akienda ofisini WCB anapigwa dolo tu! Hapo yeye mwenyewe akajiongeza kujua kazi haipo tena.

Kwa mujibu wa Mwarabu, hakupewa barua ya kusitishiwa ajira wala kuambiwa hata kwa mdomo. Alishangaa tu kuona kimya. Naye kwa vile ni mpole, akaamua kunyamaza na kuacha maisha yaendelee. Akitumia hoja hakuwahi kusaini mkataba wa ajira na Diamond wala kampuni yake ya WCB.

Ni kweli kutosaini mkataba ni sababu ya kuachishwa kazi kienyeji? Jibu ni hapana. Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ambayo inatambulika kama Sheria Kuu ya Ajira, inatambua mikataba ya aina tatu; maandishi, mdomo na mazingira.

Kwamba upo mkataba ulioandikwa, lakini kuna ambao ni wa kutamkiana kwa mdomo. Hakuna maandishi yoyote ila mazungumzo ya mdomo yanajenga mkataba. Vilevile inawezekana kukawa hakuna maandishi, wala hakukuwa na kuambiana mdomoni kuhusu mkataba, lakini mazingira yakathibitisha uwepo rasmi wa mkataba.

Nilizungumza na Mwarabu, alikuwa na mengi yenye kuumiza. Kwanza alisema alikuwa analipwa Sh500,000 tu kwa mwezi. Aliondoka anadai mishahara ya miezi mitatu, yaani Sh1.5 milioni. Nikawaza; Mwarabu alijisikiaje kuona Diamond anagawa magari ya kifahari ya Sh400 milioni, wakati yeye aliondoka kazini akiwa na kinyongo cha Sh1.5 milioni tu?

Kisa kingine, Mwarabu alisema aliuguza mtoto wake, akawa anahitaji Sh300,000 za kulipia gharama za matibabu hospitali. Alikwenda kuomba kwa Diamond amkopeshe na angemkata kwenye mshahara wake, lakini hakumpa. Kwa mujibu wa Mwarabu, gharama za matibabu ya mtoto wake alisaidiwa na shemeji yake. Nikajiuliza; Mwarabu alipoona magari ya Tanasha na Mama Dangote alikisikiaje?

Bila shaka ameumia sana. Si unajua tena kinyongo cha kibinadamu? Sh1.5 milioni malimbikizo ya mishahara miezi mitatu, Februari mpaka Machi, umeiacha kwa shingo upande, halafu unashuhudia huyohuyo ambaye hajakulipa hizo fedha anatumia Sh400 milioni kugawa magari. Mwarabu akisema hajaumia atakuwa anaongopa.

Ni kibinadamu tu; ulimwomba mtu akuazime Sh300,000 ulipie gharama za matibabu hospitali mtoto wako atibiwe na akukate kwenye mshahara wako, lakini anakwambia hana. Siku zinapita, mtu huyohuyo anatumia Sh400 milioni kuwanunulia magari mama yake na mpenzi wake. Hata kama kweli siku ulipomwomba hakuwa nazo, lakini kibinadamu roho itauma. Hivyo, hatuwezi kuongopeana, ni wazi matumizi ya pati la besidei za Tanasha na Mama Dangote, yamemuumiza Mwarabu na mwingine yeyote mwenye manung’uniko kama yake dhidi ya Diamond.

Advertisement