NYUMA YA PAZIA: Tumuulize Traore, nyumbani ni wapi?

Saturday October 10 2020

 

By EDO KUMWEMBE

ALIANDIKA Mwanafalsafa mmoja ‘…Nyumbani ni pale historia yako inapoanzia..” Mwingine akaongeza ‘..Nyumbani sio mahala, ni hisia..’ Akatokea mwingine akaongeza ‘Nyumbani ni pale ambapo mtu ameanzishia mambo yake….’

Mtoto mmoja mweusi aliyezaliwa Kusini Magharibi mwa Barcelona katika jimbo la Catalunya mapema wiki hii, alikuwa na kazi ya kutuambia nyumbani kwake ni wapi. Hakuna Mzungu mweusi. Kama ambavyo hakuna Mweusi aliye mzungu.

Adama Traore Diarra alikuwa ana kazi ya kutuonyesha nyumbani kwake mapema wiki hii. Nyumbani kwake ni wapi hasa? Alizaliwa eneo la Llobregat na wazazi wake weusi kutoka nchi ya Mali ambao walizamia Barcelona kusaka maisha miaka mingi iliyopita.

Utotoni alikuwa anazurura katika mitaa ya Barcelona. Kwao alikuwa anakwenda likizo tu. Utotoni Wahispaniola wakamuita katika timu zao za vijana. Baada ya hapo wakakaa kimya kirefu na kumsahau. Majuzi wakamuita tena katika timu ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 24.

Wahispania walikuwa wanajiandaa kucheza na Ureno, Uswisi na Ukraine. Hapo hapo Mali nao wakamuita. Mali wanacheza na Ghana na Iran katika mechi za kirafiki. Adama akatakiwa atoe majibu ni wapi atacheza. Walikotoka wazazi wake au alipozaliwa na kukulia?

Hapa ndipo nilipokumbuka majibu ya Wanafalsafa. Na hapa ikaja mada nyingine. Kwanini baadhi ya mastaa wa Afrika wanapokumbwa na hali kama hii wanaamua kucheza Afrika au katika timu za taifa za Ulaya? Inatokana na sababu tofauti.

Advertisement

Riyad Mahrez, Kalidou Koulibaly, Pierre-Emerick Aubameyang wameamua kuchezea timu za taifa za Afrika, ingawa wasingekosa nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa. Kwanini waliamua kucheza huku na sio kule?

Inawezekana kule wanaishi katika Jumuiya za Waafrika wa mataifa yao. Wanajisikia nyumbani zaidi na wanajisikia wapo karibu na mataifa yao kwa sababu kila wakiamka wanajikuta wamezungukwa na watu wa mataifa yao ya asili. Hapa wanajihisi wapo nyumbani, ingawa wamezaliwa nchi za watu.

Lakini kuna wengine ambao wamezungukwa na tamaduni zote za nchi husika waliyozaliwa. Kama ni Hispania basi unajikuta ukijisikia kuwa Mhispanioala zaidi kutoka na kutozungukwa sana na watu taifa lako la Afrika au tamaduni za Afrika.

Wakati mwingine usiipuuze sababu hii. Kusafiri mara kwa mara kumenionyesha namna ambavyo kuna Waafrika wanajihisi Waafrika zaidi hata kama wamezaliwa na kukulia Ulaya na kuna watu wa Waafrika ambao wanajiona wazungu zaidi.

Nadhani Adama alikuwa anajisikia hivi zaidi kwa sababu kuna sababu nyingine ambayo inawafanya watoto wa Kiafrika waliopo Ulaya kutochezea mataifa hayo. Ni pale ambao wanaitwa katika timu za vijana halafu inachukua muda mrefu kuitwa katika kikosi cha wakubwa.

Kwa mfano, Adama alicheza katika vikosi vya vijana lakini amelazimika kusubiri mpaka umri wa miaka 24 kuweza kuitwa katika kikosi cha wakubwa. Wenzake wengine wanatumia nafasi hii kutangaza kuchezea nchi zao za Afrika ambako baba zao walizaliwa.

Adama hakutaka kutumia nafasi hii kwa sababu mbili. Ama kwa sababu anajiona ni Mhispaniola zaidi au alikuwa na uhakika kwamba siku moja angeitwa katika kikosi cha nchi husika. Kwa Hispania ni ngumu kuchukua chaguo la pili kwa sababu wachezaji kama kina, Mikel Arteta hawakuwahi kugusa timu ya taifa.

Lakini sababu nyingine ambayo inamfanya mchezaji asubiri ni ukweli kwamba anaona atakuwa na nafasi kubwa katika dili zake za baadaye za biashara ya soka. Kwa mfano, ni wazi kuwa mchezaji wa kudumu wa timu ya taifa ya Hispania ana soko kubwa katika masuala ya uhamisho kuliko mchezaji wa kimataifa wa Mali. Labda kama huyu mchezaji wa Mali awe Didier Drogba au Samuel Eto’o.

Inawezekana Kalidou Koulibaly bado anacheza Napoli kwa sababu aliamua kuichezea timu ya taifa ya Senegal. Kama angekuwa ni beki wa kimataifa wa Ufaransa si ajabu angekuwa timu kubwa zaidi kama Samuel Umtiti, Aymeric Laporte au Raphael Verane.

Nadhani Adama ameona itakuwa ni fursa kubwa zaidi kwake kama ataamua kuchezea timu ya taifa ya Hispania. Atakuwa na nafasi kubwa ya kucheza katika michuano ya Euro na ile ya Kombe la Dunia, hivyo itamtangaza zaidi.

Ni ngumu kwa Mali kucheza Kombe la Dunia. Wanachoweza kukupa ni kushiriki katika michuano ya Mataifa ya Afrika ambayo haitazamwi sana kama ilivyo katika michuano ya Euro. Labda hili lilimfanya asubiri nafasi yake katika kikosi cha Hispania kwa misimu mingi zaidi.

Lakini nikukumbushe tu kwamba kuna suala la pesa. Mtoto mwingine aliyeamua kuichezea timu ya taifa ya Hispania ni Ansu Fati. Inadaiwa alipewa pesa na Wahispanioala ili achague kuichezea timu yao ya taifa baada ya kunyatiwa na taifa la Ureno ambalo lilikuwa linamnyatia kutokana na asili yake. Ansu Fati alizaliwa katika taifa la Guinea-Bissau ambalo limetawaliwa na Ureno.

Mwingine ambaye aliwahi kununuliwa na Wahispaniola ni Diego Costa. Wakati ule alipochagua kuichezea timu ya taifa ya Hispania kiongozi mmoja kutoka Shirikisho la Soka la Brazil, CBF alidai kwamba Costa alikuwa amepewa pesa kuichezea timu ya taifa ya Hispania na kuitosa Brazil. Kiongozi huyo alidai kwamba Costa hakuwa na sababu ya kuichezea Hispania kwani alikuwa amekwenda mkubwa na pia hakukuwa na mshambuliaji wa Brazil ambaye angemud kumuweka benchi kwa wakati huo.

Advertisement