NIPE NIKUPE : Pasi za bao la Gundogan simulizi

Muktasari:

  • Katika michuano mingine, hii sio mara ya kwanza kwa Manchester City kufunga bao ambalo limetokana na pasi nyingi uwanjani ambazo hazijaguswa na adui. Tayari ilishafanya hivyo katika pambano la Kombe la Ligi dhidi ya West Brom Oktoba mwaka jana.

MANCHESTER, ENGLAND.MANCHESTER City juzi Jumapili ilitisha. Sio tu iliwachapa wapinzani wao wa jadi wa Jiji la Manchester, Manchester United kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 lakini pia ilikuwa inatishia rekodi nyingine za United.

Bao la tatu ambalo lilifungwa na staa wa kimataifa wa Ujerumani, Ilkay Gundogan lilitokana na pasi 44 za wachezaji wa Manchester City kabla ya mpira kufikia katika mguu wake na kumfunga kiurahisi kipa mahiri wa United, David de Gea.

Nusura bao hilo lifikie bao ambalo United ililifunga Septemba 2015 katika pambano dhidi ya Southampton kupitia kwa Juan Mata baada ya wachezaji 45 wa Manchester United kupigiana pasi. Ilikuwa ni katika utawala wa kocha aliyepita, Louis van Gaal.

Katika michuano mingine, hii sio mara ya kwanza kwa Manchester City kufunga bao ambalo limetokana na pasi nyingi uwanjani ambazo hazijaguswa na adui. Tayari ilishafanya hivyo katika pambano la Kombe la Ligi dhidi ya West Brom Oktoba mwaka jana.

Katika muundo wa bao hilo, wachezaji wote wa Manchester City waliugusa mpira huku wengine wakijrudia mara kadhaa na kutimiza idadi ya pasi 52 kabla ya staa wa kimataifa wa Ujerumani hajamalizia kwa kufunga bao murua. City ilishinda mabao 2-1.

Timu nyingine ambayo iliwahi kupiga pasi nyingi zilizoelekea bao ni Liverpool ambayo katika pambano la robo fainali Kombe la Ligi 2014 dhidi ya Bournemouth ilipiga pasi 51 kabla ya staa wake wa wakati huo, Raheem Sterling hajafunga kwa urahisi. Tofauti katika pambano hili kuna wachezaji wa Liverpool hawakugusa mpira.

Kabla ya pasi za juzi za Manchester City zilizosababisha bao la Gundogan au pasi za Manchester United mwaka 2015 zilizosababisha bao la Mata, rekodi ya bao lililotokana na pasi nyingi kwa mujibu wa wataalamu wa takwimu lilifungwa na Nacer Chadli wa Tottenham.

Kwa mujibu wa Opta ambayo imeanza kukusanya takwimu hizo msimu wa 2010-2011, Chadli ambaye kwa sasa anakipiga Monaco ya Ufaransa alifunga bao hilo katika pambano dhidi ya QPR Agosti 2014 baada ya kumalizia kazi nzuri ya pasi 48 za wachezaji wenzake.

Kwa msimu huu timu nyingine ambayo imepiga pasi nyingi zilizosababisha bao ilikuwa ni Arsenal katika pambano lake la pili la msimu dhidi ya Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge ambapo bao lao la kusawazisha lililofungwa na staa wa kimataifa wa Nigeria, Alex Iwobi lilitokana na pasi 18 za wachezaji wake. Arsenal ililala 3-2.

Arsenal pia ilipiga pasi 15 kuelekea katika bao lake la kusawazisha pambano dhidi ya Liverpool lilofungwa na staa wake wa kimataifa wa Ufaransa, Alexandre Lacazette huku mpira ukiwa umeanzishwa na kipa wake, Bernd Leno.