N’Golo Kante roho kwatu kisa kawafunga Man City

Muktasari:

  • Jina la Kante lilikuwa kwenye orodha ya waliotikisa nyavu kwenye mechi hiyo ambapo The Blues walitibua rekodi ya Man City ya kutopoteza kwenye ligi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Bao lingine la Chelsea lilifungwa na David Luiz.

LIVERPOOL, ENGLAND.KIUNGO N’Golo Kante amesema amefurahi baada ya kufunga bao lililochangia ushindi muhimu wa Chelsea iliyoupata mbele ya Manchester City kwenye Ligi Kuu England juzi Jumamosi uwanjani Stamford Bridge.

Jina la Kante lilikuwa kwenye orodha ya waliotikisa nyavu kwenye mechi hiyo ambapo The Blues walitibua rekodi ya Man City ya kutopoteza kwenye ligi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Bao lingine la Chelsea lilifungwa na David Luiz.

“Kitu muhimu kwangu ni kuweza kutoa mchango mkubwa ndani ya uwanja,” alisema Kante, ambaye ni staa wa kimataifa wa Ufaransa.

“Nakuwa na furaha sana ninapoona jina langu limeingia kwenye orodha ya wafungaji na hilo ni bao langu la pili msimu huu. Tumekuwa na nyakati ngumu, lakini ukweli ni tumetaabika pamoja na tumepambana pamoja na mavuno yake ni haya mabao mawili.

“Tumefurahia ushindi huu. Unaleta hisia nzuri. Nadhani wale wenzetu ni timu bora England. Haya ni matokeo mazuri baada ya kipigo kile cha Jumatano iliyopita. Tunaamini tutaendelea kuwa hivi katika mechi zijazo.”