Mzungu azuia dili la Kagere, Okwi

Saturday December 8 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

MASHABIKI na mabosi wa Simba huwaelezi kitu kwa mastraika wao watatu pale mbele, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco kutokana na kuifanya shughuli yao ya kufunga mabao kwa uaminifu mkubwa.
Mastraika hawa ndio wanaotegemewa na Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems katika kuipa timu yake matokeo bora uwanjani, lakini kuna tarifa ambazo kwa sasa zimeanza kuwaumiza kichwa. Ndio! Okwi ambaye thamani yake sokoni kwa sasa ni Sh 396 milioni ikiwa imepanda kutoka Sh 264 milioni ambayo Simba wanatajwa kuilipa wakati wakimrudisha Msimbazi.
Hata hivyo, thamani ya Okwi inaweza kuongezeka maradufu kutokana na kiwango chake uwanjani hivyo, dili lolote kwa sasa na Simba kuifanya akaunti yao kunona.
Kwa upande wa Kagere ambaye alitua Msimbazi kwa dau la Dola za Marekani 60,000 (zaidi ya Sh 120 milioni) wakati wakimnasa kutoka Gor Mahia ya Kenya, thamani yake kwa sasa imepanda na kufikia Dola 90,000 (zaidi ya Sh 200 milioni) na huenda
ikaongezeka tena kama ataendeleza makali yake ya kupasia nyavuni.
Tangu amejiunga na Simba, Julai mwaka huu, Kagere ameifungia timu hiyo mabao 16, saba katika Ligi Kuu Bara, matatu katika Kombe la Kagame, matatu kwenye mechi za kirafiki na mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika na moja kwenye Ngao ya Jamii.
Hata hivyo, mastraka hawa wawili wapo kwenye rada za klabu tishio barani Afrika, AS Vital ya DR Congo ambayo inamtaka Kagere na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, ambayo tayari imetuma ofa kwa mabosi wa Msimbasi kutaka huduma ya Okwi.
Wiki iliyopita, Mtendaji Mkuu wa Simba, Crecentius Magori alilithibitishia Mwanaspoti kuwa, ni kweli mabosi wa Chief
wametuma ofay a kumtaka Okwi. Pia, akaenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba, kuna ofa tatu mezani kwake ambazo zote zinataka huduma ya Okwi.
Lakini, taarifa za Okwi na Kagere zimemfikia Aussems, ambaye ameweka bayana kuwa ni suala gumu sana kuwaruhusu mastraika hao kuondoka klabuni hapo kwa sasa.
Amesema suala la wafumania nyavu wake hao kutakiwa na klabu zingine limekuja kwa kushtukiza na kwamba, wakati huu Simba inajipanga kusaka matokeo mazuri kwenye michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara.
Alisema ili Simba ama klabu yoyote inayoshiriki michuano mikubwa na ligi yenye ushindani ipate matokeo mazuri ni lazima iwe na wachezaji aina ya Okwi na Kagere ama wenye uwezo zaidi ya hao.
Hata hivyo, Mbelgiji huyo amesema kwa sasa amejikita zaidi katika kukinoa kikosi chake ili kuweza kupata matokeo mazuri na kutetea ubingwa pamoja na kufanya kweli kwenye michuano ya kimataifa.
Pia, amesema masuala yote ya usajili kwa wachezaji wapya wanaoingia ama kutoka litaendelea kubaki kwa viongozi wake na kwamba, jukumu lake ni kushauri na kupendekeza.
"Tupo katika mashindano ya kimataifa ili kutimiza malengo ya timu kucheza hatua ya makundi, si rahisi kufanikiwa bila kuwa
na wachezaji wenye uwezo kama Kagere na Okwi ambao, watakuwa wakishirikiana na wenzao kusaka matokeo mazuri.
"Tangu nimefika Simba nimekutana na wachezaji wazuri ambao, nina imani kubwa wanafanya kazi kwa uaminifu na kujituma sana ili kufikia malengo tulijiwekea msimu huu.
"Huwezi kuwa na mchezaji ambaye anafanya vizuri kisha akaondoka kwenye wakati kama huu, ni ngumu sana kwani timu ina kiu ya kufanya vizuri," alisema Aussems na kuongeza:
"Kwangu nafasi ya Kagere na Okwi kuendelea kubaki kikosini bado ipo, lakini si vizuri kuzungumzia masuala ya mchezaji
mmoja mmoja na hizo taarifa za kuondoka kwao nawaachia viongozi.”

Advertisement