Mzuka wa Yanga wamtisha Dalali

Muktasari:

Kikosi cha Simba kinachoshika nafasi ya tatu, kina pointi 27, kutokana na michezo 13, huku watani wao wana alama 38 kwa michezo 14, jambo ambalo limemfanya Dalali ashindwe kujizuia akiamini kama Simba itazubaa inaweza kutemeshwa taji mapema.

YANGA ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, sawa na Azam wanaowafuata nyuma yao, lakini kasi hiyo ya mabingwa hao wa kihistoria nchini imemtikisa mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali.
Dalali alisema pengo la pointi 11 lililopo baina ya timu yake na vinara hao ni shida na kuwataka viongozi wa sasa wa klabu hiyo kufanya kitu ili wamalize kazi kibabe.
Alisema viongozi na hasa benchi la ufundi la Simba ni lazima lihakikisha kattika mechi zao saba zilizosalia kabla ya kumalizika kwa duru la kwanza wavune alama zote 21 ili wakirudi duru la pili wawe na kazi ya kula sahani moja na Yanga.
Simba iliyopo nafasi ya tatu ina pointi 27 kutokana na michezo 13, huku watani wao wana alama 38 kwa michezo 14, jambo ambalo limemfanya Dalali ashindwe kujizuia akiamini kama Simba itazubaa inaweza kutemeshwa taji mapema.
"Jambo la kwanza ni kushinda mechi saba zilizosalia, kisha tuwe kitu kimoja itakuwa rahisi kujua wapinzani wetu wana mbinu gani, wanachama wasimame kwenye nafasi yao, viongozi wafanye kazi yao, kocha awajibike na hata wachezaji pia wajitoe."
"Pointi walizotuzidi Yanga tusizichukulie rahisi, ni lazima tupunguze na kuwanasa watani, muhimu timu icheze na kufunga mabao mengi zaidi na tuhamasishane kuhakikisha kila mechi tunashinda hakuna namna nyingine," alisema Dalali aliyeweka rekodi Simba ya kunyakua taji bila kupoteza msimu wa 2009-2010.