Mzozo wala hana mpango wa kusajili

Muktasari:

  • Pia, Mzozo alimwaga sifa kwa mkongwe, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ambaye ni kinara wa kufumania nyavu kwenye kikosi hicho hadi sasa akiwa amefunga mabao manne katika mechi saba walizocheza.

KOCHA wa Friends Rangers, Herry Mzozo amesema hatasajili mchezaji hata mmoja katika dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufungwa Desemba 15.

Mzozo alisema ana hazina kubwa ya kikosi cha vijana ambao wana uwezo wa kupambana kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo.

“Sioni sababu ya kutafuta wachezaji wengine wakati kuna vijana wa U-21 wanahitaji nafasi na wana uwezo kama wengine,” alisema Mzozo.

Aliongeza atawapandisha vijana sita baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye usajili wa dirisha kubwa lililopita.

Pia, Mzozo alimwaga sifa kwa mkongwe, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ambaye ni kinara wa kufumania nyavu kwenye kikosi hicho hadi sasa akiwa amefunga mabao manne katika mechi saba walizocheza.

“Kuna timu tatu za Ligi Kuu zimeonyesha nia za kumtaka mchezaji huyo lakini hakuna barua wala mazungumzo ya kiofisi yaliyofanyika hadi sasa,” alisema Mzozo.

Kwa mujibu wa Mzozo timu zinazomsaka mkongwe huyo ni Biashara United pamoja na African Lyon na Friends wapo tayari kumwachia mchezaji huyo kama atapata ofa yoyote ile.