Mzimu wa Zahera watua kwa Mayanja

Saturday November 9 2019

Mzimu - Zahera -watua- Mayanja-KMC- klabu-Kocha- Jackson- Mayanja - Shirikisho -Afrika- Pyramids- Misri-Mwanaspoti-Soka-MwanaspotiGazeti-

 

By Mwandishi wetu

ULE mzimu wa fukuzafukuza makocha imehamia kwa Mganda Jackson Mayanja baada ya klabu yake ya KMC kutangaza kusitisha mkataba naye ikiwa ni miezi michache tangu impe mkataba wa mwaka mmoja kuinoa, akiwa ni kocha wa sita msimu huu kuachana na timu zao.
Mayanja aliyewahi kuzinoa Kagera Sugar, Coastal Union na Simba amesitishiwa mkataba wake ikiwa ni siku chache tu, tanya Yanga nao kufanya kama hivyo kwa aliyekuwa kocha wake, Mwinyi Zahera.
Zahera aliyekuwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja, alisitishiwa mkataba wake Jumanne ya wiki hii baada ya Yanga kutolewa Kombe la Shirikisho Afrika na Pyramids ya Misri.
Katika taarifa iliyotolewa mapema leo na kusainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya klabu ya KMC, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni inayoimiliki timu hiyo, Benjamin Sitta ni kwamba maridhiano ya pande mbili ndizo zilizoamua waachane kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili sasa.
Katika msimu uliopita ikiwa chini ya Kocha Etienne Ndayiragije, timu hiyo ilimaliza ya nne na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ambapo hata hivyo ilitolewa mapema na AS Kigali katika raundi ya awali, huku katika ligi ikipata matokeo yaa ovyo.
Katika mechi nane ilizocheza timu hiyo imevuna alama nane tu ikishinda michezo miwili na sare mbili, huku ikipoteza nne.
Kabla ya kutangazwa kwa ataarifa za Mayanja kusitishiwa mkataba, kocha Mayanja alikuwa nje ya benchi la ufundi kwa madai ya kukosa vikali vya kazi na ilielezwa alikuwa ameandika barua ya kuachana na timu hiyo, kwani hakuona mustakabali wake, japo uongozi wa KMC ulikuwa ukipiga danadana kuzuga kwamba bado itaendelea kuwa naye.
Mayanja anakuwa kocha wa sita katika msimu huu kuachana na timu yake baada ya Athuman Bilal 'Bilo' aliyetimuliwa baada ya mechi moja tu akiwa na Alliance, Amri Said 'Jaap Stam' aliyeachana na Biashara United, Fred Felix Minziro aliyekuwa Singida United, Malale Hamsini aliyetemeshwa kibarua Ndanda na Mwinyi Zahera aliyekuwa Yanga.
Kwa sasa taarifa za chini chini zinamtaja Patrick Aussems huenda akafuata kutokana na mabosi wa Msimbazi kukosa imani naye na kukubaliana kuachana naye lakini wakipingana kama wamuache sasa ama baada ya msimu kumalizika kwani kocha huyo Mbelegiji aliyewapa taji la pili msimu uliopita mpaka sasa hajafanya vibaya sana kwani Simba ipo kileleni na alama zao 22.

Advertisement