Mziki wa Ambokile washtusha TPL Bara

Muktasari:

Eliud Ambokile wa Mbeya City ni mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara kwa mwezi uliopita wa Septemba,

MCHEZAJI Bora wa Ligi Kuu Bara kwa mwezi uliopita wa Septemba, Eliud Ambokile wa Mbeya City ameshtusha wengi kutokana na kasi aliyoanza nayo katika ligi hiyo aiwa ndiye kinara wa mabao mpaka sasa akiwafunikia nyota kibao wa ndani na wa kigeni.

Straika huyo aliyekuwa kinara wa mabao wa City msimu uliopita kwa kufunga tisa, hadi sasa amefunga mabao sita katika mechi tisa, jambo lililopmfanya Kocha Mkuu wake, Ramadhani Nsanzurwino ashindwe kujizuia, huku akimjaza upepo ili atishe zaidi.

“Ambokile wa sasa yuko vizuri sana lakini kikubwa ambacho ninamwambia kila siku asimame katika kiwango hicho sababu wengi wao huwa wanaibuka, lakini mwisho wa siku wanajisahu na kurudi nyuma,” alisema Nsanzurwino raia kutoka Burundi japo ana asili ya Afrika Kusini.

Alisema kikubwa kwa straika huko kukomalia nidhamu na kutobweteka kwani ligi ndio kwanza imeanza.

“Kitu kikubwa ambacho, Ambokile anatakiwa kufanya ni kuwa na nidhamu ya mazoezi na hamu ya kutokubali kushindwa kwa kufanya zaidi mazoezi atafanikiwa kwani katika soka hakuna uchawi zaidi ni kufanyia kazi unachoelekezwa na bidii ya mazoezi.”