Mziba aeleza ufundi wa Said Mrisho

Muktasari:

  • Nguli huyo alisema katika mechi hizo mbili, yeye na Mrisho ‘Zico wa Kilosa’ walifunga mabao hayo katika mazingira magumu ya mechi hizo katika miaka ya 1980.

Dar es Salaam.Mshambuliaji nguli wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abeid Mziba amesema Said Mrisho ‘Zico’ alikuwa hodari wa kufunga mabao uwanjani.

Mrisho alizikwa juzi wilayani Kilosa, Morogoro, alifariki dunia Jumanne wiki hii kwa maradhi ya vidonda vya tumbo.

Mziba alisema Mrisho alikuwa hodari wa kufunga na anakumbuka mechi mbili walizoshinda kwa mbinde ambazo Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Tukuyu Stars, Reli ya Morogoro.

Nguli huyo alisema katika mechi hizo mbili, yeye na Mrisho ‘Zico wa Kilosa’ walifunga mabao hayo katika mazingira magumu ya mechi hizo katika miaka ya 1980.

“Mrisho nilimpokea Yanga na Abubakari Salum, alikuwa akicheza namba tisa mimi 10 au wakati mwingine tulibadilishana, hakuwa na mambo mengi uwanjani zaidi ya kufunga,” alisema Mziba.

Alisema Mrisho alikuwa na uwezo wa kumiliki mipira, kujiamini na alikuwa na uwezo wa kupambana na mabeki waliokuwa tishio enzi hizo. Mziba aliyekuwa hodari wa mabao ya mpira wa kichwa, alisema Mrisho alikuwa mchezaji mwenye kipaji ambaye Taifa halitamsahau.

“Katika mpira tumepoteza mtu muhimu ambaye mawazo yake katika soka yalihitajika, nakumbuka namna Mrisho alivyokuwa anajiamini na mwenye akili ya soka,” alisema Mziba.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanasoka Veterani Nchini (UMSOTA), Paul Lusozi alisema alikuwa akisumbuliwa na vidonda vya tumbo.