Mziba: Serengeti Boys wasituangushe AFCON

Muktasari:

  • Alisema kocha anayefundisha timu hiyo, hatakiwi kuridhika mapema na kujiamini ana vijana wapambanaji awaandae wachezaji kisaikolojia kwamba wanaingia kupambania nchi na kuandika rekodi ambayo itaacha alama nzuri kwao na taifa.


MCHEZAJI wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba, amesema maandalizi wanayofanya Serengeti Boys yaendane na ukubwa wa mashindano wanayotarajia kushiriki na wao wakiwa mwenyeji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mziba alisema nafasi waliyopewa ili kuonyesha thamani na umuhimu waliopewa wanatakiwa kuwa na kikosi kitakacholeta ushindani kwa timu zinazotarajia kushiriki ili kuonyesha utofauti.

Alisema kocha anayefundisha timu hiyo, hatakiwi kuridhika mapema na kujiamini ana vijana wapambanaji awaandae wachezaji kisaikolojia kwamba wanaingia kupambania nchi na kuandika rekodi ambayo itaacha alama nzuri kwao na taifa.

“Timu zote zinaandaliwa kwa mazoezi kikubwa ninachokumbusha hapa ni kuona mwalimu anawaandaa kushindana na sio kukubali kushindwa tunafahamu uwezo wa Serengeti ulivyo mkubwa lakini hatutakiwi kuwaamini kwa kuwapa mashindano makubwa kama hayo bila kuwaandaa inavyotakiwa na kuwajaribu kwa michezo ya krafiki,”

“Mashindano yamebakiza siku chache lakini bado sijasikia kama kuna michezo ya kirafiki ya kujipima nguvu ni muda huu wa kufanya hayo, ili kuendelea kuwajengea uimara nyota wetu ukiangalia michezo ya kirafiki waliyocheza Uturuki hawakuwa na kiwango kizuri, wanatakiwa sawa kufanya marekebisho ya makosa yao,” alisema Mziba.