Mziba: Ilikuwa raha iliyoje tulipomuua mnyama

Monday March 11 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abeid Mziba anasimulia jinsi hali inavyokuwa wanapoifunga Simba, pia wanapofungwa na timu hiyo.

"Aisee asikwambie mtu, uwa inakuwa hali ya huzuni mno, hata kuamka asubuhi unajiuliza mara mbili mbili."

Anasema kwa wachezaji pale wanapofungwa na Simba wachezaji wanakuwa katika hali ya majonzi mno.

"Sijui sasa hivi wachezaji wanakuwaje, lakini wakati ule sisi tukifungwa, unahisi kila mtu anakutazama au kukusema wewe kuwa ni moja ya sababu za kufungwa, yaani acha tu ndiyo sababu nasema hizi mechi zinakuwa kwenye kumbukumbu sana.

Anasema hakuna furaha iliyoje kwa wachezaji kama kuifunga Simba, hasa ukiwa miongoni mwa waliosababisha ushindi huo, yaani furaha yake uwa aielezeki.

"Yaani baada ya mechi kwanza ulali, tulikuwa tunaenda muziki au sinema, ilikuwa tumeshinda utakwenda Sikinde, yaani ilikuwa ni raha mno, asikwambie mtu kuifunga Simba kuna raha yake," anasimulia.

Maisha yake Ndani ya Yanga yalikuwaje?

Mziba anasema katika maisha yake ya mpira hakuwahi kujutia kucheza Yanga, kwani ni klabu ambayo aliishi kwa raha.

"Nilikuwa na maisha mazuri Yanga, sababu nilikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo, sikupata shida, sababu ilikuwa ni mchezaji ambaye kama sichezi, basi wachezaji wenzangu watakuna vichwa kunikosa.

Amtaja kocha bora kwake

"Nimepitia kwa makocha wengi kama Ander Helela Mbrazil, kulikuwa na kocha Mjerumani, makocha wazawa, marehemu Abdarhaman Juma, Salehe, Masudi, Ramadhan Shaban Mhinda, lakini kila mmoja alikuwa na vionjo vyake, lakini kipindi kizuri kwangu ilikuwa nilipokuwa na Mhinda.

"Yeye alicheza mpira kwa kiwango kikubwa, kizuri tu, amtoka kucheza halafu akaja kuwa kocha, hivyo akikuelekeza unamuelewa, ilikuwa nikikaa naye ananipa moyo kuwa unaweza," anasema.

Alikuwaje hadi kupewa jina la Mganga maarufu?

Huku akicheka, Mziba analikumbuka jina lake la utani la Tekelo ambalo lilikuwa jina la mganga wa kienyeji maarufu.

"Jina la Tekelo ni jina langu ambalo nimelizoea na ninazeeka nalo, mtu akiniita Tekelo najua kabisa huyo ananifahamu vema, nimelizoea na ninalipenda na ukiniita Tekelo naitika.

Anasema hilo jina alipewa na Isihaka Hassan kama utani, likakuwa na wachezaji wenzake wakawa wanamuita hivyo mazoezini, wala hakuchukizwa nalo, alilipenda na mpaka sasa analitumia.

"Unajua jina hili limetokana na historia yangu ya mpira, kuna wakati tunaweza kubanwa, lakini tukipata kona basi lazima nifunge na matokeo yanakuwa 1-0.

"Au wakati mwingine nikifunga goli mwanzo, basi alirudi sana sana tutaongeza jingine, hivyo ikawa imezoeleka hivyo, wachezaji wakiona nimefunga bao la mapema basi wanaamini kabisa goli halirudi na kweli inatokea hivyo hadi mpira unakwisha.

"Kumbe Isihaka alikuwa ana noti hicho kitu, siku moja akatania tu, akasema huyu Mziba buana anafunga magoli ya Kitekelo Tekelo tu, kuanzia hapo nikaanza kuitwa Tekelo, jina likakua hadi sasa.

Anasema kwenye mechi, mazoezini ndiyo ilikuwa jina lake, lile la Mziba likapotea, hata mtaani likazoeleka, hivyo naye alilifurahia na mpaka sasa hata akiitwa saa 7 Usiku jina hilo anaitika.

Kwanini aligoma kuichezea Simba?

Mziba anasema wakati anakwenda Yanga, alichelewa kusaini mkataba hivyo alipofika akakuta nafasi yanga zimejaa, lakini Simba kulikuwa bado kuna nafasi za usajili.

"Simba walinifuata, wakati ule ndiyo walikuwa wakijiandaa kwenda Brazil, hivyo wakanishawishi nijiunge nao, sikuwa na mapenzi na Simba, hivyo nikaamua niisubiri Yanga.

Afungiwa na Fifa kimizengwe

Mwaka 1988, Mziba anasema yeye na Athuman Chama (Marehemu), walikwenda Uarabuni kucheza soka, lakini ilikuwa ndivyo sivyo.

"Kipindi cha nyuma tulikuwa tunaondoka tu, ukipata ofa unafanya mipango yako unaondoka, lakini kwa bahati mbaya kwangu na Chama haikuwa hivyo.

"Tulikuwa tunapitia Nairobi, lakini tulipofika Namanga, pasipoti zetu zikawa zimezuiliwa, basi tukarudishwa Dar es Salaam, baada ya wiki, nikarudishiwa pasipoti yangu, nikafanya taratibu zangu nikaondoka tena.

"Ile nimefika tu Oman kwenye ile klabu iliyonichukua, nilipofanya mazoezi tu siku ya kwanza ikaja taarifa kuwa nimefungiwa na fifa mimi pamoja na Chama.

Anasema licha ya taarifa hiyo, alindelea kubaki kwenye hiyo klabu ingawa hakuwahi kucheza Ligi ya kule zaidi ya kuitumikia kwenye mechi za kirafiki.

"Nilikaa mwaka mmoja kule, ile klabu iliendelea kunilipa mshahara kama kawaida hadi msimu ulipokwisha nikaondoka kurudi Tanzania," anasema.

Anasema alipotua tu nchini, siku hiyo hiyo akafunguliwa na siku iliyofuatia Yanga ikawa inacheza Dar es Salaam na African Sports na yeye Mziba alicheza Yanga ambapo walifungwa 2-1 na bao la kufutia machozi la Yanga alifunga yeye Mziba.

Anasema hajui ni sababu gani ilikuja taarifa kuwa amefungiwa na aliporudi tu akafunguliwa kucheza soka, ingawa anaamini hakukuwa na uhakika kwani hakukuwa na kopi ya Fifa kuwa amefungiwa, zaidi ya barua tu kutoka chama cha mpira Tanzania kuwa Fifa imemfungia, lakini hakukuwa na ushahidi huo wa Fifa.

Ashawishiwa kubadili uraia

Mziba anasema klabu hiyo ya Oman baada ya ya kuwa amerejea nchini walimfuata wakitaka kumsajili tena, lakini wakamshawishi abadili uraia na awe raia wa Oman lakini ndoto yake ilififishwa na mechi ya Bonanza.

"Nilikuwa nimekubaliana nao, kwani walitaka wafanye mpango nipewe uraia wa muda kule, nilitaka tufanye kama mkataba labda baada ya miaka kadhaa halafu narudisha uraia wangu, kwani walinihitaji, lakini walipokuja kwa mara ya pili ndipo wakanikuta nimeumia.

 

 

Kumbe huyu ndiye alififisha ndoto yake kisoka

Mziba anamtaja kipa John Busoloo wa AFC Leopards kuwa ndiye alififisha mipango yake ya soka na ndiye amechangia aache soka mapema.

"Nilikuwa na mipango endelevu ya kisoka, lakini kipa huyu ndiye alitibua ndoto zangu," anasimulia.

Anasema wakati kipa huyo anamuumiza, alivuruga mipango yake mingi kwani ndicho kipindi ambacho alikuwa amepata ofa Uarabuni, lakini pia kuna mzungu alimfuata kwenda kufanya majaribio Ubelgiji.

"Huyo mzungu alikuja akanikuta nimeumia, kwani ndiyo nilikuwa nimetoka kufanyiwa upasuaji, hata Uarabuni sikuweza kwenda kwani uwezi kwenda kwenye nchi za watu ukiwa hauko fiti.

"Ilinichukua kama miezi sita nikiuguza majeraha hadi kurudi katika hali ya kawaida," anasema.

Anasema kipa huyo alimchezea faulo baada ya kufanikiwa kufunguka goli kwenye bonanza la timu za Afrika Mashariki na Kati, ilikuwa n faulo mbaya, na hata Yanga haikuweza kufika mbali kwani hawakufika nusu fainali.

"Nilipopona, niliendelea kubaki Yanga hadi 1992 anilipocheza Ligi mara ya mwisho na mwaka uliofuatia nikastaafu soka.

 

 

Katika familia yake kuna aliyefuata nyayo zake za soka?

 

Mziba anasema hakuna mtoto wake hata mmoja aliyefuata nyayo zake kisoka.

 

"Simlazimishi mwanangu yoyote kucheza soka na hakuna aliyependa, sijui kwanini," anasema.

Anasema zamani soka halikuwa na fedha kama sasa, hivyo hajanufaika nalo, kwani wakati ule walicheza kwa mapenzi, walifurahia tu kucheza mpira, lakini hawakupata fedha kama ilivyo sasa.

Analionaje soka la Tanzania hivi sasa

"Tunajitahidi kukimbia, lakini bado, mpira ni programu ndefu, bila wahusika kuzisimamia na kuachia watu wengine ni tatizo, bado tunahitaji kunyanyuka na kutoka hapa tulipo.

Anasema bado nafasi ipo kama viongozi wataamua, lakini pia wachezaji kujitoa kweli kweli, wasiridhike na hapo walipo.

Akizungumiza nafasi ya Taifa Stars kufuzu kucheza Afcon, Mziba anasema fursa hiyo ipo kama wachezaji wakiamu.

"Bahati nzuri tunacheza nyumbani, hiyo ni faida moja wapo katika kuhakikisha tnashinda, cha msingi kwanza tushinde mechi hiyo (itachezwa Machi22)halafu ndipo tutakuja kusikilizia matokeo ya Cape Verde na Lesotho," alisema Mziba.

Advertisement