Mzee Tegete awapa ushauri mzito mabosi Mbao FC

Saturday March 23 2019

 

By MASOUD MASASI

MWANZA. WAKATI Mbao FC ikiwa tayari limetangaza Benchi la Ufundi linalongozwa na Salum Mayanga,Kocha Mkongwe nchini John Tegete ameionya timu hiyo tabia ya kubadilisha makocha kwani  iko siku itakuja kuwagharimu.

Mayanga ambaye atakuwa akisaidiana na Fulgence Novatus wamejiunga na Mbao FC ambapo wamesaini mkataba mfupi utakaomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Timu hiyo ilianza kunolewa Ligi Kuu na Kocha Ettiene Ndayiragije ambaye alitimuliwa kisha akapewa kazi Amri Said“Stam”ambaye naye aliondoka na nafasi yake akapewa Ally Bushiri na sasa amekabidhiwa  Mayanga.

Akizungumza na Mwanaspoti,Tegete alisema tabia ya kubadilisha makocha inayofanywa na klabu ya Mbao iko siku itakuja kuwagharimu Ligi Kuu na wanatakiwa kuiacha.

Alisema ni jambo la ajabu sana kwa msimu mmoja kubadilisha makocha watatu kitu ambacho alisema kila mwalimu anakuja na mfumo wake ambao anataka ufuatwe  kitu ambacho kinawachanganya wachezaji.

 “Kila Kocha ana mfumo wake wa ufundishaji kwa hiyo akija anakuja na utaratibu wake sasa ndani ya msimu mmoja wamebadilishwa watatu hivi kweli hapo si kuwachanganya wachezaji”alisema Tegete.

Tegete alisema sasa viongozi wa Mbao wanatakiwa kumpa muda kocha Mayanga ili aweze kukisuka vyema kikosi hicho katika mechi zilizobaki za Ligi Kuu.

Alifafanua  kuwa  viongozi wa Mbao wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa makocha wanawapa majukumu ya kukinoa kikosi chao kwani mpira una mambo mengi.

“Timu inapofanya vibaya ni lazima muwe wavumilivu na kujua tatizo liko wapi inawezekana halipo kwa Kocha labda wachezaji hawajalipwa mishahara au kuna kitu wanadai hivyo ni muhimu kuwa na subira kwanza”alisema Kocha huyo.

MWISHO………..

Advertisement