Mzee Dalali kupokewa kishujaa na matawi ya Simba

Friday January 12 2018

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. BAADHI ya viongozi wa Matawi ya Simba kutoka Dar es Salaam na Tanga, wamemuomba mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo, Hassan Dalali, awatembelea na awaeleza mwendendo wa timu yao.

Kelele za mashabiki hao ni kutokana na Simba kupoteza nafasi ya ushiriki kombe la FA pamoja na Kombe la Mapinduzi, lakini pia haijachukua ubingwa wa ligi kuu kwa misimu mitano sasa.

Mwenyekiti wa tawi la Cheche za Simba lililo Mbagara Kingugi Dumba jijini Dar es Salaam, Said  Seif  Likepapa anasema, lengo la kumuita Dalali ni kutokana na jinsi ambavyo aliongoza kwa mafanikio enzi zake.

"Tumejipanga kumpokea kifalme kwani kila timu inapofanya vibaya, tunakumbuka busara zake namna ambavyo alifanya timu isiwe na migogoro,"anasema Likepapa.

"Timu ikifungwa wanachama wanatufuata majumbani, tunatukanwa mbele ya watoto na wake zetu, wanadhani hatufikishi malalamiko yao,maana hatuna jibu la kuwapa la kwa nini timu inafanya vibaya, naamini wakizungumza na Dalali mwenyewe ana hekima ya kutufanya tukawa pamoja na mshikamano wa kutovunjika moyo."

Mwenyekiti wa tawi la Simba Pangani, Omary Bwaza anasema enzi za Mzee Dalali hawakuwa na maumivu kama sasa ambapo wanaona ni kama kupwa na kujaa hawaelewi mstakabali wa timu hiyo kama ina taswira ya ubingwa.

"Tumemuomba Dalali kwa heshima yake aje atutembelee huku Pangani, ili angalau atupe mawili matatu, maana hata wakati anaongoza ilikuwa kawaida yake kuja kutusikiliza na kuchukua maoni yetu, hatujui kwa nini Simba inafanya vibaya wakati ina wachezaji wa maana,"anasema.

Kwa upande wa Dalali anasema, anajiandaa kufanya ziara katika matawi ya mikoa yote ya Tanzania, lengo ikiwa ni kuhamasisha umoja na mshikamano.

"Nimepigiwa simu na viongozi wa matawi mbalimbali na mikoa mbalimbali, sitaki chochote bali ni kuhakikisha wanachama hawaichoki timu yao,"anasema Dalali.