VIDEO: Mzee Dalali atia neno dua ya MO

Friday October 12 2018

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali 'Mzee Dalali' amesema ni jukumu la kila Mwanasimba kutenga muda na kufanya maombi ili mfadhiri wao Mohammed Dewji apatikane akiwa salama.

Dalali anasema ameguswa na kitendo hicho, lakini anaamini serikali ya Tanzania ni sikivu na inapenda amani, hivyo kazi yao wao itakuwa dau wakisubiria mkono wa sheria kufanya kazi yake.

"Nipo hapa makao makuu ya klabu ya Simba maalumu kwa kumuombea dua Mo kama mzazi ama binadamu, nimeshtushwa na jambo hilo, uwezo wangu unaishia kwenye dua na kuviacha vyombo vya dara vifanye kazi yake.

"Ukimzungumzia Mo kwanza anaisaidia Simba, kupitia yeye vijana wengi wana ajira, mtu wa watu na kubwa zaidi familia yake inahitaji kuwa pamoja naye kwa ajili kupanga maendeleo yao kimaisha, nina imani mwenyenzi Mungu ataweka mkono jambo hili na mwenzetu ama kijana wetu atakuwa salama," anasema Dalali.

Wanachama waliojitokeza makao makuu ya klabu hii ni wa jinsia zote na rika tofauti tofauti, huku wote wakiwa na sura za huzuni ilipoanza dua majira ya saa nane na nusu mchana.

Utulivu ulikuwa umetawala kwa upande wa wamama wakiomba kimoyo moyo, huku upande wa wanaume wao wakiomba kwa kupokezana.

Baada ya kupotea kwa Bilionea huyo, Serikali inaendelea na uchunguzi kuhakikisha wanampata na kumuondoa katika mikono ya watu hao wasiojulikana.

Viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba pamoja na mbuzi wawili wameingia ndani ya ukumbi tayari kwa kusoma dua ya kumuombe Mohammad Dewji 'MO' apatikane akiwa salama.

Advertisement