Mzambia mpya apewa mikoba ya Makambo

Muktasari:

  • Mchezaji Maybin Kalengo amepewa jezi namba 19 iliyokuwa ikivaliwa ndani ya Klabu ya Yanga

Dar es Salaam. Yanga imeanza maandalizi ya msimu mpya kwa kuweka kambi mkoani Morogoro kujiwinda na Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Vigogo wa klabu hiyo wametuma taarifa za wachezaji katika Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lakini baadhi wamekabidhiwa jezi muhimu zenye rekodi nzuri ndani ya klabu hiyo.

Yanga imewasilisha majina ya wachezaji 26 likiwemo la mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Maybin Kalengo, aliyepewa jezi namba 19 iliyokuwa ikivaliwa na nyota wa kikosi hicho, Heritier Makambo.

Makambo, raia wa DRC ameuzwa katika Klabu ya Horoya ya Guinea na ameondoka akiwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao 17 akishika nafasi ya tatu kwa ufungaji katika Ligi Kuu nyuma ya Meddie Kagere wa Simba aliyefunga 23 msimu uliopita.

Kalengo atakuwa na kazi ngumu ya kuthibitisha ubora wake uwanjani ili kuweza kuifikia au kuipiku rekodi ya Makambo kutokana na ukubwa wa jezi hiyo ndani ya klabu hiyo.

Makambo aliondoka Yanga akiwa amefunga mabao 10 kwa mpira wa kichwa, sita ya mguu wa kushoto na kulia akifunga bao moja.

Issa Bigirimana aliyetokea APR ya Rwanda amepewa jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na aliyekuwa nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu aliyetua Simba.

Ajibu akiwa Yanga alifunga mabao sita, huku akitoa pasi za mwisho 17 za mabao. Mshambuliaji Sadney Urikhob wa Namibia, ingawa bado hajawasili, atavaa jezi namba 17 iliyokuwa chini ya himaya ya Amissi Tambwe.

Naye mshambuliaji Juma Balinya, raia wa Uganda amepewa jezi namba 18 ambayo haikuwa na mtu katika msimu uliopita huku Patrick Sibomana akikabidhiwa jezi namba tisa.

Mabeki, Lamine Moro, raia wa Ghana amepewa namba 25 na Mrundi Mustapha Selemani akikabidhiwa namba 15.

Beki wa kushoto Muharami Issa atavaa jezi namba mbili iliyoachwa na Gadiel Michael aliyejiunga na Simba wakati Ally Ally atavaa namba 14.

Kiungo Abdulaziz Makame atatumia jezi namba 21 iliyokuwa ikivaliwa na Juma Mahadhi ambaye jina lake halipo katika orodha ya wachezaji watakaocheza Ligi ya Mabingwa Afrika huku Ally Sonso akipewa jezi namba tatu.

Kipa Mkenya anayepigiwa hesabu za kuwa namba moja, Farouk Shikalo amepewa jezi namba moja, ilhali Metacha Mnata akikabidhiwa namba 30.