Mwinyi Zahera: Hapa ukweli tu ,uongo mwiko

Wednesday November 6 2019

Mwinyi- Zahera- Hapa -ukweli tu-uongo mwiko-kocha-Yanga, Mwinyi -Zahera -

 

By Thobias Sebastian

KUNA wakati ilionekana kama kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye kibarua chake kimekoma rasmi jana kuwa asingeweza kudumu ndani ya kikosi hicho.

Wachambuzi wa soka la Bongo waliuona mwisho wa Zahera kutokana na tabia yake ya kusema ukweli bila kupepesa macho, jambo ambalo lilikuwa na manufaa kwa wengi japo kwa upande wake ilikuwa ni kujiweka kikaangoni.

Zahera aliyetua nchini Aprili 20, mwaka jana na tangu wakati huo amekuwa akisifika kwa kusema ukweli hata kama utakuwa mchungu kwa wengine, lakini yeye ndio keshausema.

Makala haya yanakupa dondoo za kauli za Zahera ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara tena hadharani hata kama ziliwahusu mabosi ama wachezaji wake ndani ya kikosi hicho.

MAKAMBO NA UGALI

Mpaka sasa Yanga inamuota mshambuliaji wake Heritier Makambo, ambaye aliuzwa kwenye klabu ya Horoya FC nchini Guinea.

Advertisement

Lakini, kuna wakati Makambo alikuwa akishindwa kuifanya kazi yake ya kupachika mabao vyema na hapo ndipo Zahera alijitokeza hadharani na kueleza sababu.

“Makambo anashindwa kuingiza goli kwa sababu ya kujiachia kwa kula sana. Anakula sana ugali ambao umemfanya kunenepa na kushindwa kucheza vizuri.”

TAMBWE NA MISOSI

Mshambuliaji Amissi Tambwe, ambaye kwa sasa anaichezea Fanja FC ya Oman naye alikutana na chungu ya Zahera kwenye msimu uliopita kutokana na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Bila kupepesa macho Zahera alimchana Tambwe akisema mshambuliaji wake huyo ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao, lakini tatizo ni kupenda kula hasa ugali na mbogamboga na kuongezekana uzito.

MAMA YAKE ANAFUNGA

Makambo ambaye alipendekezwa usajili wake na Zahera, alikutana tena na kauli ngumu kutoka kwa Mkongomani huyo ambaye anajiandaa kuelekea zake Ufaransa au DR Congo. Nyota huyo wa zamani wa Yanga alikutana na kauli nzito kutoka kwa Zahera baada ya kukosa mabao ya wazi kwenye mchezo dhidi ya Ndanda FC uliomalizika kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Baada ya mchezo huo Zahera alisema: “Kwa mabao ambayo Makambo ameyakosa hata mama yangu mzazi kule nyumbani Congo anaweza kufunga, nashangaa Makambo anashindwa kuifungia timu mabao.”

YANGA WALIKWENDA NA WATOTO

Wakati Zahera anatua Yanga msimu uliopita ilikuwa inacheza Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, na ilikuwa na kibarua cha kucheza na timu za USM Alger (Algeria), Gor Mahia (Kenya) na Rayon Sports ya Rwanda.

Mara baada ya kurudi kutokea Algeria kucheza na USM Alger ambapo Yanga walifungwa mabao 4-0, Zahera alisema walikwenda na watoto kucheza na timu kubwa. Alisema wachezaji wengi waliosafiri na timu kucheza na timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi hawakuwa wanajiamini kitu ambacho kilisababisha kupoteza mechi hiyo.

Wakati huo Yanga waliwakosa nyota wake kadhaa akiwemo Kelvin Yondani, Obrey Chirwa ambaye kwa sasa yupo Azam na Papy Kabamba ‘Tshishimbi’ ambao taarifa kutoka kwa uongozi wa Yanga ilielezwa kuwa walikuwa na matatizo binafsi.

ATEMA UBINGWA

Wakati wapenzi na mashabiki wengi wa Yanga wakiamini chama lao linakwenda kubeba taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya 28, kumbe jambo hilo kwa Zahera lilikuwa tofauti kabisa. Baada ya ligi kumalizika alieleza kuwa licha ya kuonyesha ushindani na kumaliza katika nafasi ya pili, malengo yake hata mkataba wake haukuwa ukionyesha kwamba alitakiwa kumaliza msimu akiwa bingwa.

Kauli hiyo huenda iliwakwaza wapenzi wa Yanga, lakini walikuja kupozwa na kauli nyingine ambayo Zahera alieleza kuwa msimu huu atasajili kikosi chenye wachezaji wa maana kwa ajili ya kubeba mataji.

TSHISHIMBI ANAKiMBIA TU

Wakati ligi ikiwa inaendelea Zahera alieleza kuwa nahodha wake Tshishimbi anashindwa kucheza katika eneo la kiungo mkabaji na muda mwingi hukimbiakimbia kama Lionel Messi ambaye anacheza klabu ya Barcelona.

Zahera alieleza kuwa mchezaji ambaye anacheza katika eneo la kiungo mkabaji anatakiwa kufikiria majukumu ya kukaba kwanza, lakini kwa Tshishimbi ilikuwa tofauti kwani alitaka kucheza kama Messi akikimbia maeneo yote ya uwanja wakati siyo jukumu lake.

KUPUNGUZA UZITO

Zahera wala hakuona tabu kuongea kauli kuwa kuna wachezaji wanatakiwa kupunguza uzito, kwa kuwa wanashindwa kucheza vizuri katika baadhi ya mechi jambo ambalo linamfanya kushindwa kuwapa nafasi ya kuitumikia timu.

Miongoni mwa nyota wa Yanga ambao walitakiwa kupunguza uzito ni Juma Balinya, Sadney Urikhob na David Molinga ambao hakusita kuwapasulia hadharani, lakini haijulikani walimchukuliaje.

UBINGWA SIMBA ‘WALIBEBWA’

Katika kauli nyingine za Zahera alieleza licha ya kwamba hakuwa na timu bora msimu uliopita kama watani wao wa jadi Simba na kutokuwa na malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi, lakini mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba walichukua ubingwa huo kutokana na kubebwa.

Zahera alieleza kuwa kama sio mambo mabaya ambayo walifanyiwa katika mechi zao za mwisho za mzunguko wa pili, Yanga walistahili kuwa mabingwa, lakini kutokana na mambo hayo walishindwa kutwaa ubingwa huo.

Advertisement