Mwinyi Zahera : Tatizo Mkwasa, usajili una shida

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalum nyumbani kwake, Zahera pia amefunguka mambo mengi akieleza hata kikosi kilichopo sasa Jangwani, sehemu kubwa hajahusika kufanya usajili zaidi ya kujulishwa kwa simu wakati akiwa mapumziko. Hebu endelea naye...!

SIKU moja tu tangu mabosi wa Yanga kutangaza kumfuta kazi aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu yao, Mwinyi Zahera, sasa amevunja ukimya na kufichua kilichomng’oa Jangwani, akidai wala sio matokeo dhidi ya Pyramids ya Misri ama yale ya Ligi Kuu Bara kama inavyoelezwa.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalum nyumbani kwake, Zahera pia amefunguka mambo mengi akieleza hata kikosi kilichopo sasa Jangwani, sehemu kubwa hajahusika kufanya usajili zaidi ya kujulishwa kwa simu wakati akiwa mapumziko. Hebu endelea naye...!

KASHTUKIZWA

Zahera anasema mpaka anakwenda Cairo, Misri hakuwa na shaka ya kutemwa na Yanga na alihakikishiwa na wakubwa zake kwamba, wana imani naye, lakini ghafla aliporejea akageuziwa kibao.

“Taarifa ya kutemwa sikuwa nayo na wala sikuwa na mawazo kusema wanaweza kusitisha mkataba wangu kwani, mwenyekiti kuna mambo tuliongea na hata jana (juzi) mkiangalia kwenye mitandao Makamu Mwenyekiti Mwakalebela (Frederick) alisema hakuna mpango wa kumuondoa kocha,” anasema na kuondelea;

“Unajua kabla sijasafiri kwenda Misri, mwenyekiti (Dk Mshindo Msolla) alikuwa Kenya alinipigia simu, kuonyesha yupo pamoja nami,” anasema.

WALIONGEA NINI NA MSOLLA?

“Baada ya mwenyekiti (Dk. Msolla) kunipigia simu akanipa pole na mambo ambayo yametokea juu ya watu wanaandika kwenye mitandao na hao ni wachache sio wote wa Yanga kuwa kocha hafai na aondolewe. Akasema sisi viongozi tunakuunga mkono kwa asilimia 101, akaniambia la pili kuwa kuna mtu mmoja alimpigia simu, ila siwezi kumtaja jina lake ni wa Yanga akamwambia kwanini uongozi haumtoi Zahera? Huyo mtu wana matatizo naye pia ninavyofahamu, Mwenyekiti akamuuliza kwanini tumuondoe kocha? Tumuondoe kwa sababu tumefungwa na Pyramids? Akaniambia akamjibu kuwa, kocha amecheza mechi nne anashinda mbili anapata sare moja na tunapoteza moja sasa nimuondoe kwa sababu ni zipi?”

“Akamwambia yeye haoni sababu ya kumuondoa kocha hata kama tunafungwa na Pyramids, hii ni klabu ambayo haiwezi kumshangaza mtu yoyote kama inaifunga Yanga hilo tukamaliza,” anaongeza Zahera.

AMTOE MWANDILA, AINGIE MKWASA

“Tulivyomaliza kuongea hilo akahamia katika jambo lingine, akasema kuna jambo nataka tuongee juu ya kocha msaidizi Noel Mwandila, Mwenyekiti akasema yeye anaona kama mashabiki wanalalamika kuwa hafai, nikamuuliza mashabiki wanasema hafai kwani wao ndio wanafanya naye kazi kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi?. Akanijibu kuwa walikuwa wanafuatilia kila wakati nikienda timu ya taifa nikirudi timu inashuka kiwango na wachezaji wanachoka haraka sana.

“Nikamuuliza timu inashuka kwa namna ipi? Nikamjibu kuwa sikubaliani na hilo kupitia takwimu tukianza na mwaka jana nilikwenda timu ya taifa na timu ikacheza karibu mechi nne tukapoteza moja tu dhidi ya Lipuli.

Akashinda na Afrika Lyon, Mbeya City na Mtibwa Sugar na hizo zote sikuwepo alibaki Noel pekee sasa timu inashuka vipi, hapo hakuwa na jibu la kuniambia.

“Safari hii nilitoka timu ya taifa tukakutana na Mbao tukashinda tena tukipata bao la ushindi kipindi cha pili, tukakutana na Pyramids kipindi cha pili tukapata bao na kama isingekuwa kosa la Ngassa (Mrisho) ina maana tungepata sare, anangalia mechi ya Polisi Tanzania walitufunga bao 3 kipindi cha pili tunarudisha zote na hapo Noel ndio yupo benchi. Nikamwambia kama timu ingekuwa inachoka labda tunaongoza tatu halafu kipindi cha pili au cha kwanza zinarudi zote hapo ningekubaliana naye na lini hilo limetokea? Mwisho akasema sasa tunafikiria kusitisha mkataba wa Noel halafu tunakuletea huyu alikuwa Katibu Mkuu, Mkwasa (Charles).

“Akaniambia alikuwa kocha msaidizi wake wakati anafundisha ni kocha mzuri atakusaidia. Nikamjibu siwezi kufanya kazi na mtu ambaye binafsi sijamchagua, nataka kufanya kazi na mtu ambaye namwamini anajua kunisikiliza nikimuagiza atafanya. Nataka nifanye kazi na mtu, ambaye unaona ni vigumu kukusikiliza utamwambia weka hii pale toa weka kule atafanya?

“Unajua kuna wakati sisi makocha tunaweza kutofautiana, najua yeye ana falsafa yake na mimi nina zangu, nikamwambia siwezi kufanya kazi na mtu, ambaye anaweza kuja na kukataa kunisikiliza nikamwambia sitaweza kukubaliana na hilo.

“Kwa hiyo maamuzi haya yamenishtua kwa jinsi nilivyokuwa naongea na mwenyekiti utaona kabisa kwamba, hujui hata hiyo kitu ilianzia wapi mpaka maamuzi haya yanafanyika tena aliniambia hata kama unafungwa na Pyramids kule hawezi kunifukuza. Utaona kama ningekubali kufanya kazi na Mkwassa basi wasingenifukuza,” alisema.

Siku 560 Yanga maisha yalikuaje?

“Maisha yangu ndani ya Yanga yalikuwa na tofauti kubwa kama kocha anavyotakiwa kuishi na timu kufuatana na jinsi nilivyofika hapa. Yanga ilikuwa na matatizo mengi na kama ningekuwa na akili ya kusema nifanye kazi kama ambavyo makocha wengine wanavyotakiwa mambo yasingekuwa mazuri. Muda mwingi nilikuwa kama mimi ndio baba wa wachezaji, wasaidizi wangu na hata timu, kuna changamoto nyingi nililazimika kuzipatia ufumbuzi ili mambo yaende vizuri na hiyo ndio kilichokuwa hapa Yanga.

“Sikuwa kocha pekee bali nilifanya na mambo mengine ambayo yanaweza kukushangaza na kama una roho nyepesi utaondoka mapema na kuacha mambo yalivyo, lakini nilivumilia kwa kiasi kikubwa ili nisiharibu mambo. Watu wengi walikuwa na imani na mimi”.

Ugumu ulikuwa wapi?

“Ugumu ulikuwa katika vitu vingi, unaingia kwenye timu unakuta kila mchezaji yuko na matatizo binafsi, unaweza kufuatwa na hata msaidizi wako anakwambia kuna msiba, kama unaweza naomba unikopeshe nauli. Unafikiria unaona hali ya klabu haiko sawa unaingiwa na huruma, lakini kubwa unataka kuona mambo yanafanikiwa hivyo, unamsaidia. Hayo sio majukumu ya kocha lakini niliamua kuyatafutia ufumbuzi ili kuleta matokeo smazuri na sio kwamba, Zahera ana pesa nyingi... hapana kulipia watu kodi za nyumba haikuwa majukumu yangu.

MICHANGO YA WANACHAMA NA USAJILI YANGA

“Wazo hili nakumbuka lilianzia Mwanza tulipokwenda kucheza mechi moja ya ligi kule, mechi ilipomalizika nikaona mbona hii timu ina mashabiki wengi halafu mambo hayaendi? Wanasema wana mashabiki wanafikia mamilioni sasa hawa mashabiki sababu ni ipi wanashindwa kuichagia timu yao wakati ina mambo magumu? Nikawa nawaza kila shabiki akitoa dola moja na kama una mashabiki 10 milioni, klabu haitapata shida tena. Baada ya kuwaza hayo nikaongea na wachezaji na ndio tukafanya ule mpango wa kutengeneza matangazao na Azam TV ili watu wachangie timu na pesa za usajili na kulipa madeni ya wachezaji.

“Ilifanikiwa naona jinsi watu walivyoitikia na wakachanga fedha ingawa sikujua ni kaisi gani kilipatikana hadi mwisho ila nashukuru lengo limetimia. Nimefariji na namna mashabiki walivyoitikia wito na kushiriki kuchangia.

KUSAJILIWA KIKOSI?

“Wakati uongozi wa Dk Mshindo Msolla unaomba ridhaa ya kuingia madarakani moja ya ahadi yake kubwa ilikuwa ni kumpa fedha za usajili ili sajili timu mwenyewe na hapa Zahera anaeleza: “Ni kweli kulikuwa na hiyo ahadi kuwa fedha za usajili zitakuwa za kutosha ana atakabidhi kwa benchi la ufundi ili kusajili wachezaji tunaowataka kwa maendeleo ya timu.

“Nakumbuka kwa mara ya kwanza nilikutana naye Iringa tuliopokwenda kucheza mchezo wa Kombe la FA, ilikuwa baada tu ya kuchaguliwa, tulikaa mezani pamoja na Noel akarudia tena akisema mwaka huu pesa zote za usajili tutawapatia ili msajili wachezaji. Mtafanya maongezi na wachezaji mnaotaka na mtakubaliana kisha mmalizane, sisi kama viongozi tutakuwa tunashuhudia tu mambo yaende sawa.

“Hali haikuwa hivyo tukasikia kuna kamati ya usajili imetengenezwa, nakumbuka kuna wakati tulipokuwa tunamsajili mchezaji wa kwanza tulifanya kikao niliwalaumu. Niliwauliza imekuwaje mnamsajili huyu mchezaji kwa pesa nyingi wakati hakuwa vizuri katika msimu uliomalizika?

“Mchezaji anacheza mechi chache anapewa pesa nyingi kuliko aliyefanya kazi kubwa, mambo hayaendi hivyo. Hapo nikawafundisha namna ya kufanya maongezi na wachezaji kama anataka kusajiliwa au hata kuongezewa mkataba mpya.

“Hapana sio wachezaji wote waliosajiliwa ni mapendekezo yangu, nayasema haya mapema ili watu wasije kusema ni Zahera. Sio kuwa sina adabu, hapana lakini lazima ukweli ufahamike kuhusiana na usajili.

“Kabla ya kusafiri kwendsa Misri kwenye Afcon, wachezaji ambao nilisema wasajiliwe ni Kalengo (Maybin), Lamine (Moro), Sadney (Urikhob), Juma Balinya na hawa wawili waliotoka Rwanda, (Patrick Sibomana na Issa Bigirimana hawa wote nililetewa baadaye nilivyorudi kutoka Afcon ndio nikamuongeza Molinga (David).”

“Hawa wachezaji wengine nilikuwa naambiwa tu kocha kuna mchezaji tunaona ni mzuri unaonaje tukimsajili, mfano mtu kama Mapinduzi Balama walikuwa wananipigia wananiambia ni mchezaji mzuri amefanya vyema, lakini haina maana kama nimemsajili mimi. Nilikuwa nawauliza mmewajuaje wakasema ni wazuri sana nikawaambia waendelee jinsi vile wanataka.

“Kuna wachezaji kama tisa hivi ambao sikuwapendekeza wasajiliwe, lakini sasa wako ndani ya timu na wengine nilisema wasisajiliwe kulingana na vile walivyocheza ligi msimu uliopita, lakini niliporudi nikawakuta wako hapa.

“Kuna usajili wa kipa wa Bandari (Farouk Shikhalo) kulikuwa na mambo mengi ni kipa mzuri, lakini shida ilikuwa bado ana mkataba na timu yake tulikutana na mwenyekiti wa usajili kule Misri akaniambia amekwenda kumaliza kazi. Nikamuuliza unamsajili sasa tunalipa pesa ngapi kwa klabu yake wakati hajamaliza mkataba, akasema mambo yatakuwa sawa kuna pesa walifuata nikawapatia baada ya kumsajili usiku nikaona mapicha.

“Baadaye Bandari FC wakabadilika wakataka pesa nyingi walifanya hivyo kwa sababu walijua Yanga wameshafanya kosa la kumsainisha mchezaji kabla ya kuongea na klabu yake na hapo nilishampigia hata mwenyekiti nikamwambia tunasajili kipa wakati tuna makipa wawili Kabwili ( Ramadhani) na Kindoki ( Klaus) tukaongeza na yule wa Mbao (Metacha Mnata) sasa makipa wote hao wanini, hakuwa na jibu katika hilo.

MWAKALEBELA HUYU HAPA

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alipoulizwa juu ya tuhuma hizo za Zahera, alisema kwa kifupi kwamba: “Kwa sasa akili yetu ipo kwenye mechi dhidi ya Ndanda na hatuna muda wa kumjadili mtu ambaye hayupo kikosini.

“Zahera hawezi kututoa kwenye reli, tunapambana kusaka ushindi kwenye mechi yetu ya Ijumaa. Alikuwapo kikosini, kama kulikuwa na matatizo kwanini hakuzungumza hadi asubiri alipotimuliwa? Hatupo tayari kumjibu ili asitupotezee dira na mipango yetu,” alisema Mwakalebela.