Mwimbaji mkongwe Vijana Jazz afariki dunia

Muktasari:

 Mazishi ya aliyekuwa kiongozi na mwanamuziki mahiri wa bendi ya Vijana Jazz, Abdallah Mgonahazeru kufanyika leo Ijumaa mkoani Morogoro.Mwanamuziki huyo alifikwa na mauti jana Alhamisi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kusumbuliwa na maradhi ya figo na kufanyiwa upasuaji wa kidole tumbo.

Dar es Salaam. Mazishi ya aliyekuwa kiongozi na mwanamuziki mahiri wa bendi ya Vijana Jazz, Abdallah Mgonahazeru aliyefariki jana atazikwa leo Ijumaa mkoani Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 04, 2019, katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) Hassan Msumari amesema mwili utatolewa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipata matibabu hadi alipofikwa na umauti na kwenda nyumbani kwake Mwananyamala Mwinjuma.
“Nyumbani unapita tu na utakaa hapo kwa nusu saa au dakika 45 kabla ya kuanza safari ya Morogoro, hapa tunaanza safari
muda si mrefu, ” amesema Msumari.
Amesema mwanamuziki huyo aliyeitumikia bendi ya vijana kwa zaidi ya miaka 20 atazikwa kijijini kwao Kinole Morogoro.
“Alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo, akapata pia tatizo la kidole tumbo na akafanyiwa upasuaji Hospitali ya Muhimbili
na jana akafikwa na mauti, ”amesema.
“Nitamkumbuka sana Mgonahazeru kwa sababu alikuwa mwanamuziki hasa, alikuwa na uchungu na muziki wa dansi na hakuwahi kuukatia tamaa, sifa yake kuu niliyojifunza ni uvumilivu,” ameongeza.
Kwa upande wake, mwimbaji Kulwa Milonge amesema amempoteza mdogo wake waliyeshibana.
“Mimi ndiyo nilimleta Vijana Jazz toka Morogoro, hakika tumepata pengo kubwa,” amesema Milonge.
Mwimbaji huyo alitingisha alipokuwa na bendi ya Vijana wakati ule alipokuwa akishirikiana na waimbaji nguli kama Jerry Nashon (marehemu) na Gotagota.