Mwili wa Tigana wapelekewa makaburini

Muktasari:

Tigana ambaye alifariki dunia, juzi katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, ameumaliza mwendo kwa kumpumzishwa jana na wachezaji wenzake wa zamani, akiwemo, aliyekuwa rafiki yake wa karibu, Mwanamtwa Kihwelo.

MWILI wa nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Ally Yusuf 'Tigana' umesindikizwa na mamia ya watu kwa ajili ya kwenda kuuzika, huku njiani wakipokewa na mamia ya wapota njia waliomuaga kiaina kiungo huyo fundi wa mpira aliyetamba Yanga, Simba na Taifa Stars.
Wakisindikizwa na kauli za 'La ilaha ila llah, Muhammad Rasulullah', waombolezaji wao walikuwa wakipokeza jeneza la mwili za Tigana wakiwa wametanda barabarani ili kulipeleka makaburini ambapo muda huu wanauzika hapa Msasani. Mashabiki wa soka, nyota wa zamani na wapya sambamba na viongozi mbalimbali walikuwa miongoni waliojumuika na ndugu na jamaa kwenye kuusindikiza mwili huo makaburini.
Tigana ambaye alifariki dunia, juzi katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, ameumaliza mwendo kwa kumpumzishwa jana na wachezaji wenzake wa zamani, akiwemo, aliyekuwa rafiki yake wa karibu, Mwanamtwa Kihwelo.
"Alikuwa mdogo wangu na sio rafiki tena. Niliinjoi kucheza naye Simba na Yanga, wakati akicheza mido ya juu nilikuwa nikizima kwa kucheza beki wa kati. Mungu amemchukua, tutakumbuka mazuri yake," alisema Kihwelo ambaye alikutana na marehemu miaka ya 90.
Tigana alizaliwa mwaka 1970 Ilala mjini Dar es Salaam na amekulia Mtaa wa Saadani huku akisoma shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ambako ndiko alianzia soka kama kipa na baadaye mchezaji wa ndani.
Timu yake ya kwanza ni Shaurimoyo Kids kabla ya kujiunga na Manyema Rangers mwaka 1989 ambako alicheza hadi mwaka 1991 alipochukuliwa na Pan Africans ikiwa Daraja la Pili (sasa Daraja la Kwanza) wakaipandisha Ligi Kuu mwaka 1993.
Mwaka 1994 akachukuliwa na Yanga SC ambako alicheza kwa msimu mmoja kabla ya kuhamia Simba SC alikocheza hadi mwaka 1997 akaenda Cadets ya Maurtius alikocheza hadi mwaka 2000 aliporejea Simba SC.  
Alicheza kwa msimu mmoja Simba SC kabla ya kurejea Yanga SC ambako alicheza hadi mwaka 2004 alipokwenda kumalizia soka yake Twiga SC ya Kinondoni.
Jina la Tigana alipewa kutokana na kufananishwa na kiungo wa kimataifa wa Ufaransa miaka ya 1980, Jean Pierre Tigana.