Mwenyekiti 'Chama la Wana' ajiuzulu

Muktasari:

Stand United walishuka daraja msimu uliopita  na mpaka sasa hawana matokeo mazuri kwenye Ligi Daraja la Kwanza  kwani wapo katika nafasi ya 10 kwenye msimamo  wakiwa na  pointi 11 baada ya kucheza mechi 10.

Shinyanga.Wakati  Stand United 'Chama la Wana' ikitarajia kufanya mkutano wa mwaka keshokutwa Jumapili,Mwenyekiti wa klabu hiyo Dk. Ellyson Maeja ametangaza kujiuzulu nafasi yake.
Mwenyekiti huyo ameiongoza Stand United katika nafasi hiyo kuanzia  Juni 2016  na ameandika barua kwenda kwa uongozi wa klabu hiyo ikieleza kuwa atakabidhi rasmi  kijiti cha uongozi kwa watu wengine Jumapili.
Maeja amesema ni kweli amefikia hatua hiyo ili aweze kuwaachia nafasi hiyo watu wengine waweze kuiongoza klabu hiyo ambayo inashiriki Ligi Daraja la kwanza ikiwa kundi B.
"Taarifa hiyo ni ya ukweli kabisa, nimejiuzulu na Jumapili katika mkutano na wanachama nitaongea yote ya moyoni ili tuweze kuisaidia klabu yetu iweze kufanya vizuri na hatimaye kuwanufaisha wanashinyanga wote" amesema Maeja.
Ameongeza kuwa baada ya kuachia ngazi atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa Stand United  na ataendelea kutoa ushirikiano pale atakapohitajika.