Mwenda ala ujeuri wake,apigwa kahasho

Muktasari:

Uchaguzi huo umefutiliwa mbali baada ya wapinzani wake Mwendwa kina Sam Nyamweya, Mosea Akaranga, Alex Ole Magelo na Ludorvic Aduda kwa kauli moja kwenda katika mahakama hiyo wakiomba uchaguzi huo usitishwe.

KAMA kuna mtu mmoja asiye na amani wala raha wakati huu, basi ni Rais wa Shirikisho la soka nchini FKF, Nick Mwendwa.

Mwendwa ambaye kwa kipindi cha miezi kadhaa amekuwa akilumbana vikali na Wizara ya Michezo akishutumiwa kwa ubadhirifu wa fedha, sasa kapigwa kahasho nzito baada ya Uchaguzi Mkuu wa FKF uliokuwa umeratibiwa kufanyika Jumamosi hii kufutiliwa mbali.

Hii ni kutokana na maamuzi yaliyotolewa na Sports Disputes Tribunal (SDT) iliyofutilia mbali sio tu uchaguzi huo mkuu bali pia chaguzi zote za matawi zilizokuwa tayari zimeshafanyika kote nchini.

Uchaguzi huo umefutiliwa mbali baada ya wapinzani wake Mwendwa kina Sam Nyamweya, Mosea Akaranga, Alex Ole Magelo na Ludorvic Aduda kwa kauli moja kwenda katika mahakama hiyo wakiomba uchaguzi huo usitishwe.

Timu hii ilidai bodi ya Uchaguzi iliyokuwa imeteuliwa na FKF kuendesha shughuli hiyo ilikuwa imejaa tu wanachama ambao wanafahamika ni vibaraka wa Mwendwa.

Pia, walipinga uamuzi wa shirikisho hilo kuwafungia baadhi ya wadau kama vile chama cha marefa nchini kutoshiriki katika shughuli hiyo kwa madai, hawakuwa wameshiriki uchaguzi wao wenyewe kwa zaidi ya miaka minne.

Msajili wa Michezo nchini (Sports Registrar) naye aliiandikia barua FKF akitaka uchuguzi huo usitishwe mpaka pale baadhi ya wadau wapigakura watakaposajiliwa na msajili hiyo.

Hata hivyo, wiki iliyopita  Mwendwa alijibu kwa ujeuri akisisitiza uchaguzi huo hauwezi kuahirishwa na utaendelea kama kawaida kutokana na gharama kubwa ambayo tayari imeshatumika kuandaa.

Sasa basi, Mwendwa na ofisi yake watalazimika kuanza upya baada ya benchi ya John Ohaga, Njeti Onyango na Mary Kimani kufutilia mbali uchaguzi huo baada ya kukubaliana na upande wa malalamishi kwamba bodi iliyoteuliwa kusimamia uchaguzi ilikuwa na kasoro.

“Tumegundua nkuwa bodi ya uchaguzi inayosimamiwa na Mwenyekiti Edwin Wamukoya na naibu wake Bi Elyanah Shiveka hakubuniwa kwa kufuata utaratibu unaofaa. Pia ushahidi umethihirisha wazi shughuli nzima za uchaguzi huu ulikuwa na udanganyifu, hila na njama hivyo umefutiliwa mbali,” SDT ilisema katika maamuzi yake.

Aidha ilisema Mwenyekiti na Naibu wake wamewahi kuwa kwenye bodi ya awali ya uchaguzi hivyo hawakupaswa kuteuliwa tena kwa mujibu wa sheria zilizopo. Vile vile wawili hao hawakupaswa kuwa kwenye bodi hiyo kwa sababu pia ni wanachama wa SDT ambayo majukumu yake ni kutatua kesi za michezo.

SDT sasa imeitaka FKF kuhusisha umaa katika uteuzi wa bodi mpya ya uchaguzi na kisha kujadiliana na wadau iliowafungia kushiriki uchaguzi kwa sababu chombo hicho kilifanya hivyo kinyume na sheria.

Hili ni pigo kubwa kwa Mwendwa ambaye alikuwa na uhakika wa kutetea wadhifa wake kiulaini. Lakini hata zaidi pigo hili limemwongezea presha kipindi ambapo akiwa anaandwama na kesi ya utumizi mbaya wa Sh244 milioni alizopewa kwa ajili ya timu ya taifa Harambee Stars ambazo stakabadhi zimeonyesha wazi alivuja hela. Katibu wa kudumu katika Wizara ya Michezo Peter Kaberia amekuwa akilumbana naye katika hili wawili hao wakiishi kushtumiana na kurushiana cheche.