Mwasisi wa Tukuyu Stars afariki dunia

Muktasari:

Mwanzilishi wa Tukuyu Stars, Ramnik Pater amefariki dunia leo asubuhi nyumbani kwake mtaa Uhindini Jijini Mbeya baada ya kugua muda mrefu.

Mbeya. Mwanzilishi wa klabu ya Tukuyu Stars mabingwa wa Ligi Kuu Bara 1986, Ramnik Patel amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake mtaa wa Uhindini kata ya Sisimba jijini Mbeya.

Marehemu Patel maarufu kwa jina la Kaka au Banyambala atakumbukwa kuiewezesha Tukuyu Stars kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara 1986, pamoja na kuwaibua wachezaji kadhaa nyota waliotamba nchini.

Msemaji wa Familia Brown Mwambinga alisema marehemu alikuwa anasumbuliwa na mguu kwa muda wa miezi minne kutokana na kuvunjika mfupa wa nyonga kwenye mguu wake wa kushoto.

Alisema awali, Marehemu Patel alilazwa katika Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo hata hivyo aliruhusiwa baada ya afya yake kuimarika na kuendelea kuugua akiwa nyumbani.

Hata hivyo alisema juzi, majira ya saa tano usiku hali yake ilibadilika ghafla hadi mauti yalipo mkuta alfajiri ya kuamkia leo.

Akizungumzia kuhusu taratibu za mazishi alisema familia inawasubiri watoto wa marehemu ambao kati yao wawili wanaishi nchini Uingereza na mwingine yupo masomoni katika chuo kikuu cha Dar-es-Salaam.

Aliyewahi kuwa kocha wa Timu hiyo,mwaka 2001 hadi 2004 Chuma Amosi alisema watamkumbuka Marehemu hasa katika mchango wake wa kuhamasisha mchezo katika Mkoa wa Mbeya.

Alisema marehemu pia atakumbukwa  kwa kuhamasisha timu nyingine za Mkoa wa Mbeya kushiriki Ligi Kuu baada ya ushindi wa Tukuyu Stars mwaka 1986

“Tukuyu Stars ndio ilikuwa timu ya kwanza Mkoa wa Mbeya kushiriki ligi kuu na kutwaa ubingwa kwa mkoani hapa, na baadae kukapelekea kuibuka kwa timu zingine kama Meko, 44 KJ, pamoja na Tiger ambayo ilikuwa ya Tunduma,”alisema

Marehemu amewacha wajane wawili pamoja na watoto watatu.