Mwanjala: Sakata la Morrison hadi saa 12 jioni limeisha

Muktasari:

Morrison, raia wa Ghana ni kama amezichonganisha klabu hizo kongwe za soka nchini.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Elias Mwanjala amesema sakata la mchezaji wa Simba, Bernard Morrison halifiki saa 12 jioni leo litakuwa limekwisha.

Mwanjala amesema wakati wowote kuanzia sasa kamati yake itakutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali.

"Sijajua ajenda zitakuwa zipi hadi nifike kwenye kikao, lakini kama ishu ya Morrison itakuwa imeletwa pia tutaijadili na kuitolea ufafanuzi leoleo," amesema.

Sakata la mkataba wa Morrison liliibuka upya hivi karibuni baada ya Yanga kudai mkataba ambao mchezaji huyo alisaini kuitumikia Simba ulikuwa na upungufu.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema mkataba huo haukuwa na saini ya klabu ya Simba zaidi ya ile ya mchezaji.

Awali, Morrison ambaye alimaliza mkataba wake wa miezi sita na Yanga, aliingia kwenye mgogoro na klabu hiyo ambayo ilidai imemuongezea mkataba wa miaka miwili huku yeye akipinga kuwa hajaongeza nayo mkataba.

Baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji kusikiliza kwa siku kadhaa kesi hiyo, ilieleza kuwa Morrison ni mchezaji huru kwani kulikuwa na upungufu wa kimkataba na Yanga, na kusajiliwa na watani zao, Simba, siku kadhaa baadaye kwenye usajili wa dirisha kubwa.

"Ishu ya madai ya Yanga juu ya uhalali wa mkataba wa mchezaji huyo na Simba nimeisikia tu kwenye vyombo vya habari, ila kama itakuwa imeletwa mezani kwetu katika kikao cha leo, basi tutaijadili na kuimaliza," amesisitiza Mwanjala.

Amesema kikao kitafanyika baadaye mchana huu na yeye yuko njiani kuelekea kwenye kikao hicho kinachofanyika Dar es Salaam.