Mwanaye Kluivert aongoza mauaji Uholanzi

Wednesday March 28 2018

 

Geneva, Uswis. Mshambuliaji nyota wa zamani wa Uholanzi, Patrick Kluivert, amevutiwa na kiwango bora cha mwanaye Justin.

Kinda huyo mwenye miaka 18, alicheza kwa mara ya kwanza timu ya Taifa ya Uholanzi dhidi ya Ureno.

Mshambuliaji huyo aliingia dakika ya 77 kuchukua nafasi ya Memphis Depay katika mchezo ambao timu hiyo ilishinda mabao 3-0 mjini Geneva, Uswis.

Kluivert alimshuhudia mwanaye akicheza mchezo huo na kuonyesha kiwango bora mbele ya mabeki wazoefu wa Ureno.

Muda mfupi baada ya mpira kumalizika, Kluivert mwenye miaka 41, aliweka video kwenye mtandao ikimuonyesha kinda huyo anavyopambana uwanjani.

“Najivunia mwanangu. Umefanya kazi nzuri. Nakupenda,”aliandika nguli huyo wa zamani aliyewika kwa kupachika mabao enzi zake.

Advertisement

Kinda huyo ameanza kunyemelewa na baadhi ya klabu za Ulaya zikitaka kumsajili majira ya kiangazi.

Miongoni mwa klabu zinazomuwinda mshambuliaji huyo ni Manchester United inayoshiriki Ligi Kuu England.

Hata, hivyo Kluivert anataka kumuona mwanaye akifuata nyayo zake kuitumikia Barcelona yenye maskani Nou Camp.

“Anafanya kazi nzuri Ajax. Ni mchezaji wa kikosi cha kwanza, anacheza utadhani amecheza muda mrefu. Ni kweli nimemuandaa kwenda kucheza Barcelona,”alisema Kluivert.

Nguli huyo alisema ana matarajio makubwa kumuona mwanaye akicheza soka kwa kiwango bora kama yeye alivyokuwa akitamba duniani.

Advertisement