Mwanaspoti yataja kikosi chake robo fainali Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Makipa wote wa timu zilizotinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wapo kwenye viwango bora kabisa, lakini katika kikosi hiki kipa David De Gea anapata nafasi ya kuanza.

JOTO lile la vipute vya hatua ya robo fainali huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya limezidi kupanda, huku mashabiki wa Manchester United wakitafakari watambebea mbeleko gani huyo mtu mfupi Lionel Messi.

Kocha wao, Ole Gunnar Solskjaer anajitutumua na kudai kwamba anaisubiri kwa hamu kubwa mechi hiyo. Kitu cha kufanya ni kusubiri na kuona vipute hivyo vitapofika.

Lakini, jambo kubwa Mwanaspoti limetazama vikosi vyote nane vilivyotinga hatua hiyo ya robo fainali na kutengeneza kikosi kimoja matata kabisa.

1.David De Gea

KIPA

(Man United)

Makipa wote wa timu zilizotinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wapo kwenye viwango bora kabisa, lakini katika kikosi hiki kipa David De Gea anapata nafasi ya kuanza.

2.Kyle Walker

BEKI WA KULIA

(Man City)

Kwenye kikosi hiki, beki wa kulia itakamatiwa na Kyle Walker wa Manchester City kutokana na kiwango bora kabisa kinachomfanya kuwa mmoja wa mabeki bora kabisa wa pembeni huko Ulaya.

3.Jordi Alba

BEKI WA KUSHOTO

(Barcelona)

Kuna mabeki wa kushoto wengi kwa timu zilizotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini Jordi Alba wa Barca hawezi kukosa namba kutokana na ubora na uzoefu wake uwanjani.

4.Matthijs de Ligt

BEKI WA KATI

(Ajax)

Beki mwenye uwezo wa kuucheza mpira, Matthijs de Ligt wa Ajax anapata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza na kuweka benchi mabeki wa kati wengine mahiri kabisa akiwamo Gerard Pique.

5.Virgil van Dijk

BEKI WA KATI

(Liverpool)

Kwenye orodha ya mabeki wa kati bora kabisa Ulaya kwa sasa Mdachi wa Liverpool, Virgil van Dijk ni mmoja wao na ndio maana hawezi kukosa nafasi katika kikosi hiki bora kabisa cha vigogo nane bora.

6.Sergio Busquets

KIUNGO WA KATI

(Barcelona)

Kwenye orodha ya viungo wa kati wenye uwezo wa kuifanya timu icheze inavyopaswa, Sergio Busquets ni moto na ndiyo maana anapata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha wababe wa Ulaya.

7.Ivan Rakitic

KIUNGO WA KULIA

(Barcelona)

Fundi wa mpira, Ivan Rakitic ni moja ya wakali wanaotamba kwenye soka la Ulaya kwa sasa na ndio maana hawezi kukosa namba kwenye chama hili la pamoja la timu zilizotinga nane bora huko Ulaya.

8.Frenkie de Jong

KIUNGO WA KATI

(Ajax)

Asikwambie mtu kuna viungo wa kati wanaobamba kwa sasa na mmoja wao ni Frenkie de Jong wa Ajax, ambaye kiwango chake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kinampa nafasi kwenye kikosi hiki.

9.Cristiano Ronaldo

MSHAMBULIAJI

(Juventus)

Staa, Cristiano Ronaldo kwenye chama hili la pamoja na timu zilizotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya atacheza kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati akiwa na jukumu moja tu, kufunga.

10.Lionel Messi

KIUNGO MSHAMBULIAJI

(Barcelona)

Supastaa wa Barcelona, Lionel Messi ni moja wa wakali wanaunda kikosi hiki akicheza kwenye namba 10 nyuma ya mshambuliaji wa kati ambaye ni Ronaldo na kufanya kikosi hiki kuwa balaa zaidi.

11.Paul Pogba

KIUNGO WA KUSHOTO

(Man United)

Kwenye kikosi cha Manchester United, Paul Pogba anapenda kucheza kiungo ya upande wa kushoto jambo linalomfanya kupata nafasi kwenye kikosi hiki cha pamoja kinachoundwa na timu nane zilizotinga hatua ya robo fainali.

Wachezaji wa akiba

-Marc-Andre ter Stegen

-Giorgio Chiellini

-Victor Lindelof

-Gerard Pique

-Luke Shaw

-Christian Eriksen

-Bernardo Silva

-Tusan Tadic

-Paul Dybala

-Sergio Aguero

-Luis Suarez

-Harry Kane

Kocha

Pep Guardiola

MANCHESTER CITY