Zanzibar yaanza Chalenji kwa sare na Sudan

Muktasari:

Kundi B la mashindano ya Chalenji linashirikisha timunne ambazo ni Kenya, Zanzibar, Tanzania Bara na Sudan

Kampala, Uganda.Timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' imeanza kwa sare 1-1 na Sudan kwenye Uwanja wa KCCA jijini Kampala katika mashindano ya Chalenji yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Zanzibar ilikuwa ya kwanza kufunga lililopatikana katika dakika ya 55 kupitia kwa Makame Hamis akihitimisha piga nikupige iliyotokea langoni mwa Sudan.

Safu ya ulinzi ya Sudan ilishindwa kuondosha hatari iliyoelekezwa na Zanzibar ambayo ilipiga kambi langoni mwao na mpira kumkuta Khamis aliyekwamisha nyavuni

Ikumbukwe kwamba Khamis alifunga bao hilo baada ya kuingia kutokea benchi akichukua nafasi ya Awesu Awesu.

Hata hivyo licha ya Zanzibar kujilinda kwa takribani dakika 35, walijikuta wakiwapa mwanya wapinzani wao kufunga bao la kusawazisha katika dakika za lala salama za mchezo kupitia kwa Montasir Yahia.

Katika mchezo huo, mchezaji Ibrahim Ilika alionyeshwa kadi nyekundu mnamo dakika ya 83 baada ya kupata kadi ya pili ya njano kutokana na faulo aliyocheza kwa mchezaji wa Sudan.