Yanga yamleta kocha Mbelgiji Luc aliyemuibua Hazard wa Real Madrid

Thursday January 9 2020

Mwanaspoti-Yanga-yamleta-kocha Mbelgiji Luc- aliyemuibua-Hazard-Real Madrid-Soka

 

Dar es Salaam. Mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo itampokea kocha wake mpya Mbelgiji Luc Eymael aliyeibua kipaji cha Eden Hazard kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera aliyetimuliwa.

Kocha Luc ameachana na Black Leopards mwishoni mwaka jana na sasa Yanga chini ya udhamini wa GSM imefanya mazungumzo naye anatarajiwa kutua nchini leo mchana kwa lengo kukamilisha ili kuchukua mikoba ya Zahera.

Kocha Luc katika mtandao wake wa Twitter aliandika leo ni siku ya kuchukua uamuzi mpya.

Mbelgiji Luc amekuwa na rekodi nzuri barani Afrika kwa klabu zake mbalimbali kufanikiwa kupata mataji katika nchi alizofundisha au kuziweka klabu zake katika mazingira mazuri katika misimamo ya ligi.

Mbali ya Leopards Mbelgiji huyo amewahi kufundisha klabu za Polokwane City na Free State Stars zote za Afrika Kusini.

Kocha Eymael alijenga heshima yake katika soka la Afrika Kusini baada ya kuibadilisha Polokwane kutoka kuwa timu ndogo na kuwa timu ya tishio kabla kutwaa ubingwa wa Kombe la Nedbank akiwa na Free State Stars 2017.

Advertisement

Mbelgiji Eymael ndiye aliyeviibua na kuvikuza vipaji vya nyota kadhaa wa Ubelgiji akiwamo Eden Hazard, Axel Witsel, Logan Bailly, Guillaume Gillet, Christian Benteke na François Sterchele.

Kocha Luc mwenye Leseni UEFA Pro na Leseni A ya CAF aliingia kufundisha soka la Afrika 2010 akiiongoza AS Vita kufika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa, pia aliweka rekodi ya kushinda mechi 23 za mashindano yote kabla ya kuachana na klabu hiyo Aprili 2011.

Mei 2011, alitimikia Gabon na kujiunga na klabu ya Missile ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa nchi hiyo na mwaka 2012 aliweka historia kwa kuisaidia timu hiyo kufuzu kwa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa pia kucheza hatua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia alisaidia wachezaji wengi wa kikosi hicho kuitwaa timu ya taifa ya Gabon pamoja na mchezaji moja kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na klabu ya FC Rostov inayoshiriki Ligi Kuu Russia.

Pia Mbelgiji huyo amefundisha ukanda wa Afrika Mashariki akiiongoza AFC Leopards ya Kenya mwaka 2013 kwa kuinusuru kushuka daraja pamoja kufuzu kwa Kombe la Shirikisho Afrika 2014, pia aliwapa ubingwa wa Kombe la FKF President's Cup.

Januari 2014, alitimikia Rwanda na kujiungana Rayon Sport na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Rwanda wakiwa wamekusanya pointi 34 kati ya 39 katika msimu wa 2013–14.

Mbali ya timu hizo pia amefundisha JS Kairouan ya Tunisia akisaidia kumaliza katika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi ikiwa ni nafasi yake ya juu zaidi msimu wa 2013-14.

Alijiunga na Al-Nasr kabla ya kutimikia Sudan ambako alijiunga na Al-Merrikh na baadaye akitimukia Afrika Kusini.

Advertisement