Yanga gari limewaka kaa mbali nao

Muktasari:

Kuhusu mifumo bado Mkwasa anapita mlemle mwa Zahera ambaye alikuwa anatumia 4-3-3 na kuna wakati alikuwa anatumia 4-4-2 ‘flati’ na ndicho anachofanya kwa sasa, mfano mechi na JKT Tanzania alitumia 4-4-2

Dar es Salaam. HUKO Jangwani kwa sasa mambo ni moto, kwani gari lao limewaka na kila kitu kimenyooka ndani ya timu yao tangu iwe chini ya Kocha Boniface Mkwasa anayekaimu nafasi ya Kocha Mkuu tangu Mkongo Mwinyi Zahera alipotimuliwa kikosini.
Mara baada ya kutimka kwa Zahera, Yanga chini ya Mkwasa ilianza kwa ushindi wa bao 1-0, baadhi ya mashabiki wa soka wakabeza wakidai waliwaotea vibonde, lakini buana wakainyoosha JKt Tanzania kwa mabao 3-2 na juzi si waliwafuata Alliance kwao jijini Mwanza na kuwafumua mabao 2-1 na kuchupa hadi nafasi ya 12 wakifikisha alama 16 kutokana na michezo saba tu.
Sasa unaambiwa mbali na timu kushinda, lakini hata wachezaji wanavyofunguka na kuupiga mpira mwingi uwanjani umewafanya baadhi ya wadau kushtuka na kuona kumbe Jangwani walikuwa wakijikaba wenyewe kipindi ikiwa na Zahera, huku pia baadhi ya wachezaji waliokuwa hawapati nafasi wakipata fursa ya kuamsha dude na wengine kubadilishiwa namba walizokuwa wakichezea enzi za Mkongoman kwa namna wanavyopewa nafasi ya kukiwasha kila wakati.

APANGUA NAMBA
Mkwasa amefanya mabadiliko kadhaa ndani ya Yanga kwa kuwabadilisha namba wachezaji na hilo limekuwa faida kwa wachache na wengine kuanza kuona mambo yanakuwa mabaya kwao, mfano, Mapinduzi Balama alitua kwenye timu hiyo kutoka Alliance FC alikokuwa anachezeshwa namba tofauti hasa namba saba na 10 ndio alionekana kuimudu zaidi.
Hata hivyo, Zahera alikuwa akimtumia kama winga ya kulia, Papy Kabamba Tshishimbi alikuwa akiibudu namba sita na nane, Zahera alikuwa akimchezesha namba 10 na sasa amerudishwa kwenye namba yake,  Ally Mtoni ‘Sonso’ beki ya kati anavyocheza sasa lakini awali alikuwa akipangwa pembeni na Jafar Mohamed naye anaonekana kupewa nafasi.
Kitendo cha wachezaji hao kurudi kwenye nafasi zao kunaifanya Yanga kuongezeka nguvu eneo la kati ambalo pia kuna, Mohamed Banka, Deusi Kaseke ambaye kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania alionyesha uwezo mkubwa na kuhusika kwenye mabao mawili lile la kwanza alilofunga, Juma Balinya pamoja na bao la tatu lilolofungwa na David Molinga.
Balinya alikuwa hana nafasi kwa Zahera na kubadilishwa kwa namba wachezaji zinawaweka mashakani baadhi ya wachezaji kuendelea kuonyesha uwezo wao akiwemo, Mrisho Ngassa, Ali Ali aliyekuwa akicheza nafasi ya beki na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutokana na uwepo wa viungo wengi ambao inaonekana Mkwasa akiwakubali zaidi. Pia beki wa Yanga, Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye bado hajarudi uwanjani namba yake nayo ipo shakani kutokana na uwezo unaoonyeshwa sasa na Juma Abdul kwa kufanya kazi nzuri uanjani.

WACHEZAJI WAMKUBALI
Kiungo wa timu hiyo, Abdulaziz Makame alisema Mkwasa anawachukulia kama watoto wake, jambo lililowajenga kisaikolojia kufanya kazi kwa kujituma na uhuru wa kuona wanawajibu mkubwa wa kuleta maendeleo ya klabu.
“Ujue kila kocha ana ujuzi wake ama wamezidiana vitu, kiufundi Yanga imeanza kucheza mpira wa pasi tofauti na mwanzo, lakini pia Mkwasa alikaa na sisi akatujengea umoja na tunamwona kama baba tupo huru kumueleza chochote na yupO huru kutukanya,” alisema.
Kwa upande wa kipa wa timu hiyo, Metacha Mnata alisema kila kocha ana mbinu zake na kuhusu Mkwasa anamuona anampa nafasi kila mchezaji kuonyesha uwezo wake.
“Kila kocha ana mbinu zake, Mkwasa katujengea umoja na kufanya kazi kwa akili ya utulivu, kilichopo ni kila mchezaji kupambania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza,” alisema.

WASIKIE WACHAMBUZI
Ally Mayay, nyota wa zamani wa klabu hiyo na mchambuzi wa soka nchini, ameitazama Yanga ya Mkwasa na kubaini kwamba kocha huyo amecheza na saikolojia ya wachezaji na timu imeongeza kujiamini na pumzi kwa sasa.
“Kuhusu mifumo bado Mkwasa anapita mlemle mwa Zahera ambaye alikuwa anatumia 4-3-3 na kuna wakati alikuwa anatumia 4-4-2 ‘flati’ na ndicho anachofanya kwa sasa, mfano mechi na JKT Tanzania alitumia 4-4-2.
“Hilo halitoshi Yanga inapaswa kutumia vyema usajili wa dirisha dogo la wachezaji kupata straika na kiungo mbunifu lasivyo wanaweza wakaja wakapata shida katika mechi za Lipuli FC, Namungo FC, Kagera Sugar na Azam FC ambazo zina wachezaji wanaojituma zaidi,” alisema Mayay.
Mchambuzi mwingine Alex Kashasha, alisema Mkwasa ana vitu vitatu muhimu, kwanza kamwaminisha kila mchezaji kama ana uwezo, kaondoa makundi na kuwajenga saikolojia. “Pia, Mkwasa hulka yake ni mpole, hilo linasaidia sana kwa tasisi kubwa kama Yanga, kwani kila jambo halichukulii kwa ‘tempa’ anafanya maamuzi yake kwa umakini, timu ilikuwa na ‘tempa’ hilo linawachanganya wachezaji kusikiliza sana maneno kuliko kufanya kazi yao. “Kaondoa makundi, mfano kama, Juma Balinya alitoka Uganda akiwa kwenye kiwango cha hali ya juu ghafla akazima baada ya kutua Yanga, Mkwasa kampa nafasi, kaonyesha kitu kwa maana ana jicho la kumpa kila mchezaji nafasi, timu inashambulia kwa sasa tofauti na mwanzo ambapo ilikuwa inajilinda sana na mabao yalikuwa yanapatikana kwa tabu,” alisema.

KAULI YA MKWASA
Alipoulizwa ni kitu gani amekibadilisha kwenye kikosi chake, kinachofanya timu kutengeneza mabao mengi tangu apokee mikoba kutoka kwa Zahera?Alijibu kwa kifupi kwamba waulizwe wachezaji.
“Sina jibu juu ya swali lako, hilo linapaswa kuwauliza wachezaji kitu gani kimewafanya wabadilike, hao ndio watakuwa na majibu mazuri na sio mimi.”