Vijana City Bulls yaiduwaza Savio yatwaa ubingwa RBA

Muktasari:

Mbali na ubingwa, Vijana City Bulls iliondoka na tuzo ya MVP, mfungaji bora, mfungaji bora wa pointi tatu na mtoaji bora wa pasi za mwisho wakati Savio ikiambulia tuzo ya mzuiaji bora.

Dar es Salaam. Vijana City Bulls imetwaa ubingwa wa Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA) kwa kuifunga Savio kwa pointi 53-51 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Indoor, Dar es Salaam.

Tofauti ya pointi mbili ziliitoa Savio vichwa chini katika fainali hiyo iliyokuwa na ushindani wa hali ya juu kutoka kwa timu zote.

Wachezaji wa Savio walinyong'onyea huku wengine wakionekana kutoamini kilichotokea katika fainali hiyo iliyopigwa kwenye uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakati Savio wakiwa wakilia kwa Vijana City ilikuwa ni shangwe kwa kocha Ashraf Haroun kwa kutawazwa kuwa bingwa mpya licha ya ushindi huo mwembamba wa pointi 53-51.

Savio ambayo mwaka 2016 na 2017 ilitwaa ubingwa mfululizo, ilishindwa kuendeleza kasi hiyo mwaka 2018 ilipovuliwa na JKT na msimu huu imeuachia kwa Vijana City Bulls baada ya kushindwa kutamba katika mchezo uliokuwa na upinzani.

Mbali na ubingwa, Vijana City Bulls iliondoka na tuzo ya MVP, mfungaji bora, mfungaji bora wa pointi tatu na mtoaji bora wa pasi za mwisho wakati Savio ikiambulia tuzo ya mzuiaji bora.

Nyota wa Vijana City Bulls, Stephano Mshana alichomoza na tuzo ya MVP wakati Jonas Mushi akitwaa tuzo ya mfungaji bora na ile ya mfungaji bora wa pointi tatu (three point).

Anthony Jeikanga aliyeondoka na tuzo ya mtoaji wa pasi za mwisho (Assist) wakati Savio ikiambulia tuzo ya mzuiaji bora (best rebounder) iliyokwenda kwa Colnelius Gabliel.

Ukonga Kings iliambulia nafasi ya tatu baada ya kuifunga Kurasini Heat kwa pointi 73-65 katika mchezo wa utangulizi jana jioni.