Vieira ajipigia debe kupewa mikoba Arsenal

Muktasari:

Arsenal kwa sasa haina meneja tangu walipomfuta kazi Unai Emery kufuatia kichapo kutoka kwa Eintracht Frankfurt kwenye Europa League

LONDON, ENGLAND.PATRICK Vieira amesema kamwe hawezi kuwakatalia Arsenal baada ya sasa kuvumishwa na uwezekano wa kwenda kukalia kiti cha ukocha kwenye timu hiyo yenye maskani yake Emirates.
Lakini, alidai kwamba kwa sasa akili yake ipo kwenye kuitumikia Nice na kudai anakoshwa na mipango ya klabu hiyo ya Ufaransa. Arsenal kwa sasa haina meneja tangu walipomfuta kazi Unai Emery kufuatia kichapo kutoka kwa Eintracht Frankfurt kwenye Europa League.
Aliyekuwa msaidizi wa Emery, Freddie Ljungburg kwa sasa ndiye aliyekabidhiwa majukumu ya kuinoa timu hiyo kwa muda wakati mabosi wakiendelea kutafuta kocha mkuu. Chini ya Ljungberg, timu hiyo ilishuka hadi kwennye nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu England kabla ya mchezo wao wa jana Jumatatu usiku ugenini kwa West Ham United.
Kuna makocha wengi wanaohusishwa na mpango wa kwenda kuinoa Arsenal, akiwamo kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino na kiungo wa zamani wa timu hiyo, msaidizi wa Pep Guardiola huko Manchester City, Mikel Arteta.
Lakini, Vieira, ambaye pia alikuwa staa wa zamani wa Arsenal alipoulizwa kuhusu kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo alisema: "Huwezi kuikatalia timu ambayo uliwahi kuichezea kwa miaka tisa."
"Lakini, kwa kusema ukweli kwa sasa nimetuliza akili yangu Nice. Najisikia vizuri kuwa hapa na kumekuwa na mipango mizuri. Siku zote nimekuwa nikisema nimekuwa mwenye furaha kuwa Nice. Tupo tunapiga kazi kwa ajili ya kuipeleka mbele klabu."