Uchambuzi: Usiku wa Simba na Yanga huwa kama hivi

Saturday January 4 2020

Mwanaspoti-Uchambuzi-Usiku wa SimbaSC- Yanga-Watani wa jadi-mechi-Kariakoodabi

 

By Ally Mayay

“USIKU wa kuamkia vita hauchelewi kucha,” kauli hii naikumbuka kwa kuwa ndio iliyokuwa ikitamkwa na wachezaji wa wakati huo kwenye usiku wa siku ya kuamika mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga.
Usiku kama wa jana Ijumaa ya Januari 3, kuamkia leo Jumamosi kuna mechi inayozikutanisha timu hizo kongwe nchini katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Nakumbuka usiku wa kuamkia siku ya mechi hiyo kwa wachezaji wakati huo tulikuwa tukiuona kama vile ni mfupi kuliko usiku mwingine wowote ule.  Na wakati mwingine huwa na utashi wa usiku huo kumalizika haraka ili ifike siku hiyo ambayo husubiriwa na wadau wengi kutoka pande zote mbili yaani za klabu hizo zenye maskani yake Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Siku zote historia itaendelea kuwa historia na mambo ya sasa yataendelea kuwa mambo ya sasa ingawaje katika kujifunza jambo lolote lile hapa duniani historia inahitajika.
 Mwanadamu hutakiwa kuanza kwenye historia ya jambo hilo kabla ya kufikia wakati wa sasa kwa kuwa historia ya jambo hilo ndio iliyosababishja jambo hilo kuwepo sasa.
 Hivyo, utani huu wa jadi ambao ni wa kihistoria ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kuifanya mechi inayozikutanisha timu hizi mbili kuwa ya kipekee sio tu kwa wachjezaji, bali hata kwa viongozi, wapenzi na mashabiki.
Nasema haya kwa sababu inawezekana hata wachezaji wa sasa ambao wanazitumikia klabu hizi nao wanakutana na nyakati kama tulizokutana nazo miaka ya nyuma.
Wakati tulipokuwa tukijiandaa na mechi kama hii ya watani wa jadi inayofanyika leo Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, mazingira kama hayo ya ‘usiku wa kuamkia vita hauchelewi kukucha’ muda wote ulitawala vinywani  mwa wachezaji. Kilichokuwa kinajadiliwa kwa muda wote ni mechi hiyo tu kuanzia kwenye eneo la chakula cha usiku hadi muda wa kuingia kitandani.
Mara nyingi wachezaji huwa katika makundi kuanzia wawili huku wakiona muda ni  mchache na unakimbia kwa kasi kuliko siku zote kuelekea  asubuhi ya siku ya mchezo wenyewe.
Hali hii ilitufanya wachezaji muda wote kuifikiria na kuizungumzia mechi hiyo tu kiasi cha kusahau mambo mengine yote. Hata kama kuna mambo yalikuwa hayajakaa sawasawa kwenye familia. Na hali hiyo ilikuwa inajengwa kuanzia nje ya uwanja kwa maana ya mashabiki, viongozi na wadau wengine. Nakumbuka hata ilipokuwa ikitokea mathalani wachezaji fulani kama hawana  viatu vya kuchezeaau  kutokuwa katika hali nzuri, matatizo kama hayo wakati huo yalikuwa yakitatulia  haraka na viongozi kueleka mechi hii tu na sio mechi nyingine hata kama ikiwa ni  dhidi ya Zamalek ya Misri au Waydad Casablanca ya Morocco au Mamelody Sundown ya Afrika kusini.
Hali hiyo vichwani kwa wachezaji ilikuwa inajenga taswira ya utofauti kati ya mechi tulizokuwa tukicheza na timu tuliyocheza dhidi ya watani wa jadi, hivyo kuichukulia tofauti.
 Ni kweli kuwa ni muda mrefu umepita tangu tulipocheza soka  miaka ya nyuma kabla ya kusataafu lakini mazingira ya mechi hizo za watani wa jadi za nyakati hizo yanaweza kuwa sawasawa na mazingira ya mechi hii inayopigwa leo.
Kwa sasa bado mashabiki na viongozi wamethibitisha kuendelea kuwa sambamba na historia ya klabu hizi kwani hufurahi zaidi pale timu yao inapowafunga watani wa jadi kuliko ikitwaa ubingwa wa wa Ligi Kuu au hata ule wa Kombe la Kagame.
Hii ni kuthibitisha kuwa historia ile bado inaendelezwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hivyo, naamini hata kwa wachezjai nao usiku wa kuamkia asubihi ya leo ulikuwa mfupi tofauti na usiku mwingine wakati timu hizi zilipokuwa zikijiandaa dhidi ya Biashara United au dhidi ya Ndanda.
Kutokana na usiku kuwa mfupi ni imani yangu mazungumzo ya wachezaji yalijikita katika mchezo husika, hivyo kuifanya akili kuwa tayari kuingia katika mchezo.  Kuingia mapema mchezoni kwa mchezaji kulikuwa na mchango mkubwa uwanjani kwakuwa kunamfanya kuwa na utayari wa mchezo wenyewe.
Hali hiyo inamfanya kuweka jitihada ambazo hubebwa na kipaji alichonacho na kuweza kufanya vizuri uwanjani.
Kutokana utayari huo wa kiakili ni matarajio yangu kuona mechi yenye ushindani kwani maandalizi  ya kiakili kwa  wachezaji  yana mchango mkubwa wa kufanya mchezo uonekane bora uwanjani. Hata kama timu yake haitapata matokeo katika mechi hiyo.
Nakumbuka pia thamini ya mchezaji katika mechi kama hizi ilikuwa inaongezeka. Kama timu imefanya vizuri zaidi baada ya mechi mchezaji hukutana na watu usiowajua lakini wanaweza kummalizia shida zake zote, hata kama ni malipo kodi ya pango la mwaka.
Hii hutokana na mchezaji kuwafurahisha mashabiki wake, viongozi na wengine asiowajua uwajani dhidi ya watani wa  jadi! N i mechi yenye hamasa ya ainba yake kwa pande zote za wachezaji  kwa kweli.
Niwatakie mechi nzuri wachezaji huku nikisubiri mrejesho kutoka kwako!

Advertisement