Wimbo wa Kapatikana wa Reunion Mapacha wazua jambo

Wednesday January 8 2020

Mwanaspoti-Tanzania-Wimbo Kapatikana-Reunion Mapacha-Twanga Pepete-wazua-jambo-bendi

 

By RHOBI CHACHA

Dar es Salaam. ‘Kuchwa kuchwaa ....Kuchwa ni shughuli pevuuu...mbaya zaidii kwa yule uliyempendaa…yeye anakondaa... wewe unanenepaa…kwa mawazoo..kwa mawazoo..leleeee...lalaaaaaa....

Hiki ni kibwagizo cha wimbo wa Kuachwa kutoka Mapacha wanne bendi, kwa mtu anayependa muziki wa dansi bongo kwa muda wa miaka 11 iliyopita hatacha kukumbuka wimbo huo uliojipatia umaarufu kwa jinsi ulivyopangiliwa sauti, vyombo vya muziki na ujumbe wenye uhalisia kwa jamii.

Bendi ya Mapacha wanne ilikuwa inaundwa na  Joseph Michael ‘Jose Mara’, Junior Kalala ‘Kalala Junior’, Khaleed Chuma ‘Chokoraa’, Charles Gabriel ‘Chaz Baba’ walitengana kabla ya kuungana upya hivi karibuni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanamuziki hao walioianzisha bendi ya Mapacha wanne wamesema Reunion Mapacha ipo kwa ajili ya matukio tu na sio shoo za kila siku.

Wamesema mbali na kuwa kila mmoja yupo kwenye bendi yake, ila hii 'project' ya Reunion Mapacha ni ya kutengeneza albam na kubwa zaidi wamelenga kufanya shoo za mikoani na wimbo huo wa 'Kapatikana' ndo wimbo wao kwanza.

"Reunion Mapacha ni sisi watu wanne tumeamua kujiunga kutengeneza kazi bila ya kuwa nyuma ya mtu au kampuni yoyote, na hadi kufikia hapa watu tunamiliki bendi na wengine washawahi kuongoza bendi kuna mtu kweli atakubali kusimamiwa kwa hiki tunachokifanya?

Advertisement

“Kiufupi hakuna mkono wa mtu Reunion Mapacha, watu wategemee vitu vizuri toka kwetu na wasihofie kuwa bendi zetu tunazomiliki hazitafanya kazi, zitafanya kazi kama kawaida," alisema Jose Mara

"Ukweli lengo la Reunion Mapacha tumeona tufanye nyimbo za pamoja ili wadau wajue hatuna tatizo kama wanavyohisi kwamba sisi tumegombana, yaani majukumu ya bendi yataendelea kama kawaida," alisema Kalala Junior

Chokoraa amesema mashabiki zetu waelewe huu wimbo wa Kapatikana ni jibu la wimbo wetu wa kuachwa, hivyo Reunion Mapacha iko kwa ajilia ya kuwakumbusha mashabiki zetu namna tulivyokuwa tukifanya wakati tupo kwenye kundi moja," alisema Chokoraa.

ASHA BARAKA ACHARUKA

Baada ya Reunion Mapacha kutuma kava ya utambulisho wa wimbo wao wa Kapatikana katika magroup ya Dansi, mmiliki wa bendi ya The African Stars 'Twanga Pepeta', Asha Baraka amepinga kitendo na wanamuziki wake Kalala Junior na Chaz Baba kushiriki kutoa wimbo huo wa Kapatikana wa Reunion Mapacha bila ya kuomba ruhusa kwa uongozi wa bendi hiyo.

"Heshima ni kitu cha bure kuwe na heshima tu ya kazi lengo ni kuinua muziki wa dansi sio mtu tu unakurupuka kufanya kitu, matokeo yake unakuja kuona wanamuziki wako kwenye mabango, matangazo kwenye magroup, kweli hiyo ni heshima hiyo?

“Twanga pepeta inaongozwa na Luiza Mbutu ambaye ni Mkurugenzi wa bendi sasa hivi na mwanamuziki mwenzenu mmeshindwa kumwambia? hana hata habari, mpaka ananiuliza mimi ananitumia kava hawa vipi mama wamekuomba ruhusa? embu acheni nyie waandaaji mnaofanya hivyo nasema humu sababu kuna waandishi na kuna wahusika ambao wako nyuma ya hii mapacha na kava inaonyesha lebo ya Clouds please naomba tuheshimiane jamani" alisikika Asha Baraka

"Nawajua sana vizuri hawa wanamuziki wangu, lazima kuna mratibu hapa hata kama leo wanatambulisha wimbo wao mpya nawajua vizuri na akili zao nazijua kuna mratibu hapa wa hawa watu na ndio maana nimesema humu, nimesema humu kwa sababu wapo watu humu wanaoohusika, hilo tatizo hakuna tatizo watoe taarifa watu wangapi wanafanya zingzong?” alisema Baraka.

Akizungumzia madai ya Baraka, Kalala Junior alisema huu ni wimbo na sio shoo kusema kwamba sijamtaarifu kuwa nina shoo sehemu fulani siku fulani, mbona huwa tunatoa sana nyimbo nje ya bendi?

“Wimbo wa Kapatikana ni wimbo kama nyingine zilizotolewa nje ya bendi, labda kwakuwa limetumika jina la mapacha ndio wasiwasi ya baadhi ya watu, na nitoe tu wasawasi kwa watu hii sio bendi, maana sisi wanne kila mtu ana bendi yake mimi bado niko Twanga na ni kiongozi wa bendi hiyo ya Twanga, nitaenda muelewesha mama Asha Baraka najua ataelewa tu, yule ni mama yetu," alisema Kalala Junior

Jose Mara alisema madai ya kusema kuna mratibu wa Reunion Mapacha hakuna kitu kama hicho, kama waratibu basi ni wao wenyewe wanne ambao wamefikiria kufanya hivyo.

 

 

 

Advertisement