Kocha Kilimanjaro Queens ahamisha darasa uwanjani

Muktasari:

Mbali na kuwafundisha kwa vitendo uwanjani makipa wake, aliwataka kuandika kisha akawapa mtihani wa kuandika.

Dar es Salaam.Kocha wa makipa wa timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Queens', Fatuma Omary aliamua kuanzisha darasa la muda kwa wachezaji wake uwanjani.

Fatuma kipa aliyedaka kwa mafanikio timu hiyo katika miaka ya nyuma aliwapa darasa la kuandika wachezaji hao.

Mbali na kuwafundisha kwa vitendo uwanjani makipa wake, aliwataka kuandika kisha akawapa mtihani wa kuandika.

Aliwafundisha mbinu za kipa na kumjua kipa ni mtu gani, lengo wajue wanachokifanya na wavishike.

"Hizo zote ni mbinu tu za kuhakikisha ninachowafundisha wanakishika na si vingine, mtu anapoandika anaweka kichwani na amekifanyia mtihani anakishika, "alisema Fatuma.

Fatuma alifanya hivyo kwa makipa wote wa timu ya wakubwa inayojiandaa na mashindano ya Chalenji Cecafa yanayotarajia kuanza hivi karibuni.