Kapombe beki aliyefanya uamuzi uliowashitua wengi

Muktasari:

Kapombe alianzia soka kwenye kituo cha Morogoro Youth na baadaye kujiunga na Polisi Morogoro, na ilikuwa ni hapo Simba ndipo ilipomnasa ambapo alikaa kwa misimu miwili kati ya 2011–2013 na baadaye kutimkia Ufaransa kwenye Klabu ya Cannes FC inashiriki Ligi Daraja la Tatu kwa sasa alikocheza michezo miwili.

MAPEMA mwezi huu beki wa Simba, Shomari Kapombe alitangaza rasmi kuacha kuitumikia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kutokana na matatizo ya kiafya, jambo ambalo liliwashitua watu wengi.
Kama utakuwa unakumbuka vizuri Kapombe tangu aumie mwishoni mwa mwaka 2018 akiwa nchini Afrika Kusini katika kambi ya Taifa Stars kujiaandaa na mchezo dhidi ya Lesotho kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2019 iliyofanyika Misri, hakuonekana tena na uzi wa Stars aliyoanza kuichezea 2011.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameitumikia Taifa Stars kwa miaka minane na kufunga bao moja, ambapo alianza akiwa anaitumikia timu ya Simba, msimu ambao chama lake hilo lilifanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kukusanya pointi 63 na kuivua ubingwa Yanga iliyomaliza nafasi ya pili ikiwa na alama 56.
Kapombe alianzia soka kwenye kituo cha Morogoro Youth na baadaye kujiunga na Polisi Morogoro, na ilikuwa ni hapo Simba ndipo ilipomnasa ambapo alikaa kwa misimu miwili kati ya 2011–2013 na baadaye kutimkia Ufaransa kwenye Klabu ya Cannes FC inashiriki Ligi Daraja la Tatu kwa sasa alikocheza michezo miwili.
Mchezaji huyo hakuwa na msimu mzuri nchini humo kwani aliamua kurejea nyumbani na kujiunga na Azam FC ambayo aliikuta imetoka kubeba ubingwa wa Ligi Kuu na kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo.
Aliitumikia Azam FC kwa misimu mitatu kuanzia 2014–2017 na kuamua kurudi Simba ambako alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu hiyo.

1 Bao pekee aliloifunga Taifa Stars kwa muda wote alioutumikia
2 Idadi ya mataji ya wa Ligi Kuu Bara, yote akibeba akiwa na Simba msimu wa mwaka 2011/12 na msimu uliopita
2 Idadi ya timu za Ligi Kuu alizochezea, Azam FC na Simba
3 Misimu ambayo aliitumikia Azam FC tangu msimu wa mwaka 2014 hadi 2017
8 Miaka ambayo ameiichezea timu ya Taifa tangu mwaka 2011 hadi 2019
12 Jezi anayovaa Simba
27 Umri wa mchezaji huyo aliyezaliwa Januari 28, 1992
2014 Mwaka ambao alitimkia Ufaransa kwenda kujiunga na Cannes FC
2018 Mwaka ambao alionekana mara ya mwisho akiwa na kikosi cha Stars
2021 Mwisho wa mkataba wake dhidi ya Simba ambao alisaini wa miaka miwili